Makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Prof. lughano Kusiluka, akizungumza mara baada ya kuhitimisha zoezi la mashindao ya utafiti wa kuimarisha elimu ya udaktari kwa afya nchini ambayo yameshirikisha Chuo Kikuu cha Oslo (UiO) cha nchini Norway, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) nchini Tanzania.
Tausi Mwakyandile aliyeibuka kinara katika mashindano hayo mwanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS)
Na Gideon Gregory, Dodoma.
Makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Prof. lughano Kusiluka amesema kupitia mashindano ya mradi wa kuimarisha elimu ya udaktari kwa afya Tanzania (DOCEHTA), wataenda kutayarisha kozi fupi mbalimbali kwaajili ya kuwajengea uwezo wanafunzi wanaosoma masomo ya uzamili ili waweze kuandika miradi mizuri ya utafiti.
Prof. Kusiluka ameyasema hayo Jijini Dodoma mara baada ya kuhitimisha zoezi la mashindao ya utafiti wa kuimarisha elimu ya udaktari kwa afya nchini ambayo yameshirikisha Chuo Kikuu cha Oslo (UiO) cha nchini Norway, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) nchini Tanzania.
“Lengo letu ni kwamba hizi kozi zitumike kwa wanafunzi wote wanaokuja kusoma hapa UDOM lakini pia tunatamani hizi kozi zifundishwe kwa wanafunzi wanaosoma kozi za uzamili katika vyuo vyote Tanzania zikisaidiana na zingine pia zinaandaliwa na vyuo vingine”, amesema Prof. Lughano.
Amesema anauhakika baada ya kukamilika kwa mradi huo kiwango cha kufundisha na kufanya utafiti ambacho kitatokana na tasilifu ya wanafunzi wao kitakuwa cha juu zaidi na kuongeza kuwa pia hilo ni lengo la nchi kutaka wahitimu kutoka vyuo vikuu nchini kuweza kufanya kazi na kukubalika popote duniani.
“Tunatamani kuwa na wengi kutoka vyuo vyetu vya Tanzania wakishindana na kushinda katika ngazi za kimataifa kwani kwasasa tumeona wizara ya elimu hivi karibuni iliweza kutoa tuzo sasa hili ndilo tunalolihitaji zaidi”, amesema.
Kwa Upande wake Tausi Mwakyandile aliyeibuka kinara katika mashindano hayo mwanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), amesema ushindi umekuwa chachu kubwa kwake kuendelea kupambana kutokana na changamoto mbalimbali alizozipitia kukamilisha masomo yake.
“Pia mimi ni mkufunzi kwahiyo nitaenda kuwasaidia wanafunzi wangu katika kufanya tafiti na kuwasilisha matokeo yao ya tafiti, kwahiyo huu uzoefu umekuwa kama fundisho kwangu na naamini nilichokipata nitaenda kuwasaidia wanafunzi wenzangu”, amesema.
Sambamba na hayo moja ya malengo mahususi ya mradi ni huo kuimarisha ubora na uwezo wa mafunzo na utafiti wa elimu ya kiwango cha PhD, kuunda fursa kwa wanafunzi wa PhD, kuwasiliana na kujihusisha na utafiti wao mbele ya hadhira anuwai ikiwa ni njia mojawapo ya kufanikisha hilo.