Kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza kikiendelea
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza wamesema baadhi ya shule za Sekondari,msingi zinaupungufu mkubwa wa madawati ambapo wameiomba Serikali kutatua changamoto hiyo ili wanafunzi waweze kusoma katika mazingira rafiki.
Madiwani hao wametoa ombi hilo Jana Jumatano Juni 12, 2024 kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza kilicholenga kupokea taarifa za utekelezaji ngazi ya kamati robo ya tatu kilichofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri hiyo.
Akizungumza kwenye kikao hicho Diwani wa Kata ya Lwanhima Marco Swalala, alisema Shule zilizoko kwenye Kata yake zina madawati machache huku idadi ya wanafunzi ikiwa ni kubwa.
“Shule ya msingi Lwanhima inajumla ya wanafunzi 1,600 madawati yako 102 hii ni kero kubwa sana kwa wanafunzi kwani wanakaa kwa kubanana na wengine wanakaa chini hivyo Serikali iangalie namna nzuri ya kuwaondolea kero hii wanafunzi ili waweze kusoma vizuri”, alisema Swalla
Akizungumzia Shule ya msingi Bugayamba iliyopo katika Kata ya Lwanhima Wilaya ya Nyamagana Mkoani hapa Swalala, alisema inawafunzi 780 huku madawati yakiwa ni 84.
Kwaupande wake Diwani wa Kata ya Kishiri Haruna Maziku, alisema Kata yake inaupungufu mkubwa wa madawati kalibia shule zote za msingi na sekondari.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza Peter Juma, alikili kuwepo kwa changamoto ya upungufu wa madawati ambapo alieleza hatua walizoanza kuzifanya kwaajili ya kukabiliana na tatizo hilo.
“Saivi tumeona tuweke muda wa masomo uwe mara mbili wanafunzi waingie asubuhi watoke mchana na wengine waingie mchana hadi jioni kwenye shule ambazo zinaupungufu wa madawati,tumeshaomba kibali Mkoani wameturuhusu tuanze”, alisema Juma.
Mwenyekiti wa kikao hicho ambae ni Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza Sima Costantine, alimsisitiza Mkurugenzi kusimamia maeneo ambayo yameonekana na changamoto ambazo zimekuwa zikijirudia ili ziweze kupatiwa utatuzi wa haraka.