Afisa mhifadhi wa shirika la kimataifa la uhifadhi mazingira(WWF)Deo Kilasara kulia,akikabidhi kwa Mkuu wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Simon Chacha,box lenye mabomu baridi yaliyotengenezwa kwa kutumia pilipili yanayotumika kufukuza wanyama wakali hususani Tembo wanaovamia makazi ya binadamu wilayani humo.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Simon Chacha kushoto,akimsikiliza afisa maliasili wa wilaya hiyo Dunia Almasi kuhusu matukio ya wanyama wakali na waharibifu wanaovamia makazi ya binadamu baada ya kupokea msaada wa vifaa mbalimbali vikiwemo mabomu kwa ajili ya kufukuza wanyama wanatoka hifadhini na kwenda kwenye makazi ya watu.
Na Mwandishi Maalum,Tunduru
SHIRIKA la Kimataifa la uhifadhi mazingira Duniani(WWF),limekabidhi vifaa mbalimbali kwa Serikali ya wilaya Tunduru na Namtumbo vitakavyosaidia katika kudhibiti wanyama wakali na waharibifu wanaotoka kwenye hifadhi na kwenda kwenye makazi ya watu.
Miongoni mwa vifaa hivyo ni mabomu baridi 2,300 ya kurusha kwa mkono yaliyotengenezwa kwa kutumia pilipili,sare kwa ajili ya askari wanyamapori wa vijiji(VGS),mahema,viatu(buti) na vibuyu vya maji msaada wenye thamani ya Sh.milioni 63.
Akikabidhi vifaa hivyo kwa Mkuu wa wilaya ya Tunduru Simon Chacha na Mkuu wa wilaya ya Namtumbo Ngollo Malenya,Afisa Mhifadhi wa WWF Deogratius Kilasara alisema,lengo la msaada huo ili visaidie kufukuza na kudhibiti wanyamapori,usimamizi na uhifadhi wa mazingira.
Alisema,WWF imesaidia mavazi maalum ya kujikinga na mvua wakati wa masika ili kuwawezesha askari hao kutekeleza majukumu yao kikamilifu na kutoa fursa kwa wananchi kuendelea na shughuli zao za kila siku ikiwemo kilimo.
Alisema,kutokana na wilaya ya Tunduru na Namtumbo kuzungukwa na Hifadhi ya Taifa ya Nyerere,kumekuwa na matukio ya mara kwa mara ya wanyama hususani Tembo kuvamia maeneo ya binadamu na kufanya uharibifu wa mali,kushambulia watu na kusababisha ulemavu wa kudumu na wengine vifo.
Alisema,askari hao watatumika kutoa elimu ya uhifadhi wa mazingira na usimamizi wa rasilimali za nchi,namna ya kujikinga na wanyama wakali na kuboresha masuala ya uhifadhi pamoja na kudhibiti changamoto ya watu kuingia kwenye mazingira yaliyohifadhiwa.
Kwa mujibu wa Kilasara,askari hao wanapokwenda kwenye jamii ili kutoa elimu itakuwa rahisi jamii kuwaelewa na kuelewa umuhimu wa uhifadhi na kupokea kwa haraka elimu ya kujikinga na wanyama wakali na waharibifu wanaovamia katika makazi yao.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru Simon Chacha,ameishukuru WWF kwa msaada unaolenga kuboresha usimamizi wa shughuli za uhifadhi na ulinzi wa rasilimali za wanyamapori hususani katika kukabiliana na wanyama wakali na waharibifu.
Alisema,wilaya ya Tunduru ni miongoni mwa wilaya zilizopata athari kubwa kutokana na wanyama wakali na waharibifu wanaovamia mashamba na kushambulia watu.
Alisema licha ya jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali,lakini ipo haja kwa wadau kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya wanyama hao kwa kutoishi au kufanya shughuli zao kwenye mapito ya wanyama.
“Elimu inatakiwa ielekezwe kwa watu wetu kuhusu tabia za wanyama na nini cha kufanya ili kupunguza kama sio kumaliza athari za wanyama hao,nadhani elimu ni kitu sahihi kuliko hata haya mabomu tunayotengeneza”alisema Chacha.
Amewataka askari wa vijiji, kwenda kuwa sehemu ya utatuzi wa matatizo ambayo wananchi wanayapata yanayosababishwa na wanyama wakali na waharibifu katika vijiji vyao wanaotoka kwenye hifadhi na kwenda kwenye makazi ya watu.
Chacha,amewataka kutumia vifaa hivyo kwa kazi iliyokusudiwa na kujiepusha kufanya vitendo kinyume na sheria na taratibu za nchi ikiwemo kupokea rushwa kutoka kwa wafugaji wanaoingiza mifugo kwenye maeneo yasiyoruhusiwa.
“kwa yeyote atakayekwenda kinyume na yale aliyoelekezwa atahesabika na kuchukuliwa hatua kama mharifu mwingine,na nyie kwa kuwa mmepata mafunzo ya uaskari hatua kali zaidi zitachukuliwa dhidi yenu”alisema Dc Chacha.
Afisa uhifadhi daraja la pili kutoka Hifadhi ya Taifa ya Nyerere kanda ya Kalulu Julius Shija alisemaTanapa kwa kushirikiana na WWF wamefanikiwa kupata vikundi vya askari katika vijiji 18 ambao watahusika katika kuzuia na kupambana na wanyama wakali na waharibifu.
Alisema,askari hao watakuwa mstari wa mbele kutoa elimu ya uhifadhi kwa vijiji wanakotoka na kufika kwa haraka kufika kwenye matukio ya wanyama wanaotoka porini na kwenda kwenye vijiji na kufanya uharibifu.