MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu ameishukuru serikali kwa kupeleka kiasi cha Shilingi Bilioni 2.4 kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA),Wilaya ya Ikungi.
Pamoja na shukrani hizo ameiomba serikali kusaidia usafiri ili kurahisisha shughuli za kiutawala katika chuo hicho.
Mtaturu ametoa ombi hilo Juni 11,2024,Bungeni Jijini Dodoma katika kipindi cha maswali na majibu.
“ Kwanza nianze kwa kumshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa ktupatia Shilingi Bilioni 2.4 kwa ajili ya kujenga Chuo bora cha VETA Ikungi,na sasa hivi tunavyoongea Chuo kimeanza kazi chini ya Mkuu wake Mathias Luhanga na wanafunzi wapo darasani,niiombe serikali kwa ajili ya mambo ya kiutawala Chuo kinahitaji usafiri,naomba kujua lini serikali itapeleka gari kwa ajili ya mambo ya kiutawala,?.amehoji.
Akijibu swali hilo Naibu Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Omary Kipanga amekiri kuwa ni kweli kwenye vyuo 25 wana changamoto ya usafiri.
“Nimuondoe wasiwasi Mbunge safari ni hatua na hatua tumeshaanza, kimsingi tumeanza kujenga majengo baadae tukatafuta watumishi kwa ajili ya mafunzo kuanza na sasa yameanza,vifaa tumeanza kupeleka na hatua inayofuata ni kupeleka vyombo saidizi kwa ajili ya kuhakikisha wataalam,walimu na watumishi wetu wanafanya kazi zao kwa ufanisi ,
“Nimuondoe wasiwasi Mbunge kuwa katika bajeti ijayo tumeweka fungu kwa ajili ya ununuzi wa magari kwa ajili ya vyuo hivi vya VETA, FDC na Vyuo vya Ualimu, tunaamini katika bajeti ya mwakani mambo yanaenda kufanyika,”.amesema.