Dar es Salaam,
Hospitali ya Mkoa Temeke inaendelea kujivunia mafanikio katika upatikanaji wa dawa na vifaa tiba, hali ambayo imeboresha huduma kwa wagonjwa. Katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu uliopita, hospitali imefanikiwa kufikia upatikanaji wa dawa kwa asilimia 98% kwa bidhaa takribani 500, huku dawa muhimu zote zikifikia upatikanaji wa asilimia 100%.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke, Dkt. Joseph Kimaro, amesema mafanikio haya yamewezesha wagonjwa kupata dawa ndani ya hospitali bila usumbufu wa kutafuta huduma nje ya hospitali. Hii imepunguza muda wa wagonjwa kupata huduma na kuleta amani kwa wataalamu wa afya wanaofanya kazi hospitalini.
Pamoja na mafanikio haya, hospitali imejenga eneo maalumu kwa ajili ya kuuza dawa kwa jamii kwa bei nafuu na zenye ubora sambamba na za hospitalini. Eneo hili linalenga kusaidia wananchi wote, hususan wale wanaotibiwa katika hospitali za jirani, kupata dawa kwa urahisi na gharama nafuu.
Aidha, Dkt. Kimaro ametoa wito kwa jamii na wadau wanaozungumza maneno tofauti kuhusu hospitali. Amehimiza kuwa wanapokutana na jambo lisilokuwa sawa, wawasiliane na uongozi wa hospitali ili changamoto zote ziweze kupokelewa na kutumika kama fursa ya kuboresha huduma zaidi.
Kwa ujumla, Hospitali ya Mkoa Temeke inaendelea kufanya juhudi kubwa kuboresha huduma za afya na kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa kiwango cha juu, na hivyo kuboresha afya za wananchi wa Temeke na maeneo ya jirani.