Afisa uhifadhi wa WWF Tanzania Deogratus kilasara,akizungumza na wanafunzi wa shule za  msingi na Sekondari walipotembelea vitalu vya miti wilayani Mbinga.

Na Muhidin Amri, Mbinga

SHIRIKA la Uhifadhi mazingira duniani World Wide Fund (WWF) limetoa mafunzo ya uhifadhi na elimu ya upandaji miti kwa  Wanafunzi wa mikoa ya Ruvuma na Mtwara, lengo  likiwa kuwapa ili kuwajengea uwezo wa kuhifadhi mazingira.

Akizungumza na Wanafunzi wa shule  za msingi na Sekondari kutoka wilaya za mkoa wa Ruvuma walipotembelea vitalu vya miche ya miti wilaya ya Mbinga Afisa uhifadhi wa WWF Tanzania Deogratus kilasara amesema, mafunzo hayo yanalenga kuwapa elimu na kujifunza masuala mbalimbali ya uhifadhi na upandaji miti kwa  kwa kuzingatia kwamba watakuwa mabalozi wazuri katika jamii.

Amesema, lengo la shirika ni kuwapa elimu  inayohusu upandaji miti kuanzia hatua ya kuandaa vitalu na miche kwani itawasaidia kuanda miti ya uhifadhi pamoja na miti ya itakayowapa manufaa mbalimbali katika jamii na  kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi.

“Tunawaandaa wanafunzi hawa kuja kuelimisha na kupambana na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na kuzuia uharibifu wa mazingira, hivyo baada ya elimu hii tunaamini uelewa wa utunzaji mazingira imerithishwa kikamilifu na italeta chachu kwa taifa” alisema kilasara.

Naye kiongozi wa msafara huo ambaye ni Kaimu Afisa Elimu wa Wilaya ya Namtumbo Osmani Mponda amesema, mafunzo hayo kwa wanafunzi ni muhimu sana kwani wao ndio wenye dhamana kwa kizazi kinachokuja hivyo kupitia mafunzo  hayo kwa vitendo yataongeza wahifadhi wengi katika jamii.

“Nimefurahi kwa kuja kujifunza namna  ambavyo tunaweza otesha miti kuanzia hatua ya mbegu hadi kufikia kuwa mche, tumejifunza mengi  suala la uhifadhi wa mazingira naomba WWF waendelee kutoa mafunzo haya mwaka hadi mwaka kwani itasaidia kuwa na mabalozi wengi wa mazingira” alisema Mponda.

Mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya sekondari Mwamba  Ibrahimu Ali amesema, kupitia mafunzo hayo atakuwa balozi mzuri wa kutoa elimu, kuelemisha na kufundisha wanafunzi wenzake namna ya kuendelea kurithisha kwa vitendo katika jamii.

“Uchafuzi wa mazingira unaweza kupelekea au kusababisha mabadliko ya tabia  ya nche ikiwemo ongezeko la joto duniani, hivyo ushauri wangu kwa WWF waendelee kuturithisha elimu hii kwa vitendo kwani sisi ndio taifa la baadaye”.

Naye Bahati Said  mwanafunzi wa kidato cha kwanza kutoka Shule ya Sekondari ya Matemanga wilayani Tunduru, amelishukuru shirika la WWF kwa kuwapa elimu ya usimamizi na utunzaji mazingira kwani kupitia wao wataendele kuyafanya mazingira kuwa salama.

“Nimejifunza masuala ya uhifadhi mazingira kwa kuona hatua zote hiyo nimekuwa balozi bora ambaye naelewa jinsi ya  uhifadhi mazingira upo hatarini kutokana na shughuli  za kibinadamu kama ukataji miti ovyo, hivyo elimu hii itatuwesha kuelimisha jamii na kuyafanya mazingira kubaki salama”.