Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Hassan Khamis Hafidh akizungumza na wanafunzi wa Saikolojia katika Mkutano Mkuu na Kongamano la wanafunzi wa kada hiyo katika vyuo vikuu vya Zanzibar lillilofanyika ukumbi wa Studio Rahaleo Mjini Unguja.
Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Hassan Khamis Hafidh akimkabidhi cheti cha shukrani Mwenyekiti wa Taasisi ya Inshirah Charitable Organization Zanzibar Kevser Kocadag katika Mkutano Mkuu na Kongamano la wanafunzi wa kada ya Saikolojia katika Vyuo vikuu vya Zanzibar lillilofanyika ukumbi wa Studio Rahaleo Mjini Unguja.
Balozi wa Vijana Mohammed Kassim akimkabidhi zawadi maalum Mwenyekiti wa Taasisi ya Inshirah Charitable Organization Zanzibar katika Mkutano Mkuu na Kongamano la wanafunzi wa kada ya Saikolojia katika Vyuo vikuu vya Zanzibar lillilofanyika ukumbi wa Studio Rahaleo Mjini Unguja.
Baadhi ya washiriki wakifuatilia Mkutano mkuu na Kongamano la wanafunzi wa kada ya Saikolojia katika vyuo vikuu vya Zanzibar lillilofanyika ukumbi wa Studio Rahaleo Mjini Unguja.
PICHA NA FAUZIA MUSSA –MAELEZO ZANZIBAR
Na Fauzia Mussa , Maelezo .
Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Hassan Khamis Hafidh amesema kuwepo kwa wanasaikoljia nchini kutasaidia jamii kuondokana na msongo wa mawazo na kuugua afya ya akili.
Akizungumza katika kongamano la wanafunzi wa Saikolojia wa vyuo vikuu Zanzibar Naibu Hafidh amewataka wataalamu hao kutumia elimu zao kuelimisha jamii juu ya athari zinazotokana na msongo wa mawazo ili kuweza kujilinda.
“Binadamu tunakabiliwa na matatizo mbali mbali kama maradhi na migogoro mambo yanayopelekea msongo wa mawazo hivyo kuwepo kwa wanasaikolojia katika maeneo yetu kutasaidia kupunguza matatizo haya.” Alieleza Naibu Hassan
Aidha ameeleza kuwa wanasaikolojia bado ni watu muhimu katika maeneo mbalimbali kwani hata wagonjwa wanaosumbuliwa na maradhi sugu, wanahitaji matibabu ya Saikolojia kuweza kukubaliana na hali hiyo.
Sambamba na hayo amewataka wanafunzi wa kada hiyo kutumia ujuzi wao kuelimisha jamii juu ya athari za matumizi ya dawa za kulevya ili kupata taifa lenye watu imara.
Amefahamisha kuwa vijana wengi wanaotoka katika vituo vya kurekebishia tabia wanarudia kutumia dawa za kulevya kutokana na kukosa matibabu ya saikolojia hivyo kada hiyo ni muhimu na inapaswa kupewa kipaombele.
“katika vituo vya kurekebisha tabia (Soba house) hakuna wanasaikolojia kuweza kuwatibu hawa wathirika wa dawa za kulevya hili linachangia wao kurudia tena katika matumizi ya dawa hizo”alisema naibu Waziri
Akitoa nasaha kwa wanafunzi hao balozi wa Vijana bw. Mohamed Kassim na Mkuu wa idara ya afya ya saikolojia kutoka chuo kikuu cha Zanzibar (ZU) dkt. khalfan Mohamed, wamesema kuna umuhimu mkubwa wa taasisi za Serikali na binafsi kuwepo wanasaikolojia ili kuwa salama katika sehemu za kazi.
Akisoma risala kwa niaba ya wanafunzi wa kada hiyo Ramadhan Mohamed Hassan amesema licha ya kozi hiyo kuwa na umuhimu mkubwa kwa jamii lakini imekua ikakabiliwa na matatizo mengi ikiwemo kutokupewa kipaombele katika nafasi za ajira.
Katika Mkutano huo mada mbali mbali zilijadiliwa ikiwemo saikolojia ya afya ya akili, ugonjwa wa msongo baada ya janga na athari za saikolojia za vitendo vya udhalilishaji kisaikolojia na ukatili wa kijinsia.