NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa, akizungumza na Wasimamizi wa Uchaguzi na Mawakala wa Vyama mbali mbali vya Siasa vilivyoshiriki Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kwanani Unguja leo tarehe 8 Juni, 2024.
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar.
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa, ametembelea vituo 31 vya Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Kwahani Wilaya Mjini, Mkoa Mjini Magharibi Kisiwani Unguja unaofanyika leo Juni 8, 2024.
Akizungumza katika vituo tofauti alisema ameridhishwa na mwenendo wa uchaguzi huo unaofanyika katika hali ya amani na utulivu.
Dkt.Dimwa, amesema wananchi wamepata fursa ya kufika katika vituo mbali mbali vya upigaji wa kura na kutekeleza haki yao ya kidemokrasia ya kumchagua mgombea mwenye sifa wanazoona anafaa kuwa Mbunge wa Jimbo hilo.
“Nimetembelea vituo vyote na kuona namna wananchi mbalimbali walivyojitokeza kwa wingi kupiga kura katika vituo vyao, tunatarajia hali hii ya utulivu itaendelea mpaka kumalizika kwa zoezi hili la uchaguzi.”, amefafanua Dkt.Dimwa.
Katika maelezo yake Dkt.Dimwa, alifafanua kuwa matarajio ya CCM ni kupata ushindi mkubwa kupitia mgombea wake Khamis Yussuf Mussa (Pele) na kwamba Chama hicho kimetekeleza vizuri ilani yake ndani ya Jimbo hilo.
Uchaguzi huo unafanyika baada ya kufariki dunia kutokana na maradhi ya shinikizo la damu kwa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo Ahmada Yahya Abdulwakil mnamo April 8, 2024.