Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2024 ukikimbizwa katika Halmashauri ya Mji Newala mkoani Mtwara ambapo umetembelea,kukagua na kufungua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo mradi wa upanuzi wa maji Makonde utakaogharimu zaidi ya Sh.bilioni 84.7 hadi kukamilika kwake.
Waziri wa nchi ofisi ya Rais na Mbunge wa Jimbo la Newala Mjini Kapteni mstaafu George Mkuchika akizungumza na wananchi waliojitokeza kupokea mwenge wa Uhuru kwenye la upanuzi wa mradi wa maji Makonde,katikati Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2024 Godfrey Mnzava na kushoto Mkuu wa wilaya ya Newala Rajabu Kundya.
Tenki lenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 6 za maji linalojengwa kupitia upanuzi wa mradi wa maji Makonde wilayani Newala ambalo ujenzi wake unaendelea.
Na Mwandishi Maalum,Newala
KIONGOZI wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2024 Godfrey Mnzava,amemtaka Mkandarasi kampuni ya China Civil Engineering Construction Corperation(CCECC) inayofanya kazi ya upanuzi na ukarabati wa mradi wa maji Makonde kuongeza kasi ili mradi huo uweze kukamilika kwa muda uliopangwa.
Mnzava,ametoa agizo hilo jana baada ya kutembelea na kukagua kazi ya upanuzi na ukarabati wa mradi wa maji Makonde unaotekelezwa kwa muda wa miezi 20 kuanzia mwezi Juni 2022 na unatarajia kukamilika mwezi Julai 2024.
Aidha,amemtaka Mkandarasi kufuata sheria,taratibu na miongozo iliyowekwa kwenye mkataba ambayo inaeleza muda wa kukamilika kwa kazi hiyo.
Amesema,Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuwaondolea kero ya upatikanaji wa huduma ya maji wananchi wa wilaya hizo mbili,hivyo ni wajibu wa Mkandarasi kuhakikisha anatekeleza makubaliano yaliyopo na siyo vinginevyo.
Amewaomba wanachi wanaoishi kuzunguka eneo la mradi,kuwa walinzi na kuwachukua hatua watu wote watakaobainika kuhujumu mradi kwa kuiba vifaa vinavyoletwa kwa ajili ya matengenezo ya mradi huo kwa lengo la kuwaondolea kero ya maji kwenye maeneo yao.
Mbunge wa Jimbo na Newala Mjini George Mkuchika alisema,kwa muda mrefu sasa wananchi wa jimbo hilo na Tandahimba hawana maji safi na salama badala yake wanatumia maji ya visima walivyochimba wenyewe ambayo sio safi na salama.
Mkuchika ambaye ni Waziri wa nchi ofisi ya Rais,amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kutoa kiasi cha Sh.bilioni 84.7 kwa ajili ya ukarabti wa mradi huo unaosubiriwa kwa hamu kubwa na wananchi kwa kuwa utakuwa suluhisho la upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa wilaya hizo mbili.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya maji Makonde Francis Bwire alisema,mradi wa maji Makonde ni miongoni mwa miradi inayofanyiwa ukarabati mkubwa ili uweze kukidhi mahitaji ya sasa kwa wananchi kupitia mradi wa maji wa miji 28.
Alisema,mradi wa maji Makonde unatarajia kunufaisha Halmashauri nne za Newala Mji, Halmashauri ya wilaya Newala,Tandahimba na Nanyamba zenye wakazi 670,000 kati yao 104,349 wanaishi katika Halmashauri ya Mji Newala na gharama ya utekelezaji wake ni Sh.84,785,044,947.74.
Mkuu wa wilaya ya Newala Rajabu Kundya,amewashukuru wananchi waliotoa maeneo yao kwa hiari ili kupisha utekelezaji wa mradi huo na kuwataka watu wengine kuiga mfano huo wa kizalendo.