Naibu Katibu mkuu wizara ya ujenzi ,mawasiliano na uchukuzi Zanzibar ,Dk.Mzee Suleiman Mndewa akifungua mkutano huo mkoani Arusha .
Posta Masta mkuu ,Maharage Chande akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano huo .
Katibu Mkuu wa PAPU Afrika,Dkt Sifundo Chifu Moyo akizungumza kuhusiana na mkutano huo.
Washiriki mbalimbali wa mkutano huo unaoendelea mkoani Arusha .
Happy Lazaro,Arusha.
Arusha .Naibu Katibu mkuu wizara ya ujenzi ,mawasiliano na uchukuzi Zanzibar ,Dk.Mzee Suleiman Mndewa amewataka Wataalamu wa masuala ya Posta Afrika kutumia vyema maendeleo ya teknolojia katika kuwezesha sekta hiyo kufungua fursa za kiuchumi na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi katika nchi hizo .
Ameyasema hayo leo mkoani Arusha wakati akifungua mkutano wa 42 wa baraza la utawala la Umoja wa Posta Afrika unaoenda sambamba na ufunguzi wa vikao vya wataalamu wa masuala ya Posta .
Aidha mkutano huo umewashirikisha Wataalamu kutoka nchi zote za Afrika wanachama wa PAPU ikiwa na lengo la kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili ili kutoa huduma bora kwa wananchi .
Dk.Mndewa amesema kuwa nchi za Afrika ili ziweze kufanikiwa zaidi katika masuala hayo ni wajibu wao kwa pamoja kama nchi hizo kuhakikisha kila mmoja anashiriki katika uchumi wa kidigitali.
“Kupitia mkutano huu ni wajibu wetu kuhakikisha tunatafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili nchi wanachama,kwani bado kuna changamoto katika nchi za Afrika ikiwemo miundombinu na teknolojia ambazo zinahitaji kupatiwa ufumbuzi ili kurahisisha mawasiliano kwa haraka”amesema Dk.Mndewa.
Ameongeza kuwa ,ni vizuri nchi za Afrika kwa umoja wao kutumia teknolojia ili kuweza kupunguza gharama na kuweza kutimiza malengo waliyojiwekea kama nchi.
Naye Posta Masta mkuu ,Maharage Chande amesema kuwa,mchango wa posta ni kuhakikisha sheria na mambo ya kiutawala yanasaidia kufanya maboresho mbalimbali katika sekta sambamba na kusaidia biashara na uchumi katika nchi za Afrika.
“Tunataka kuzungumza kwa karibu na kuangalia namna tutaweza kufanya biashara kwa urahisi kutoka kusini kwenda kaskazini na tunataka kuhakikisha kanuni zinafuatwa katika kufanikisha biashara hiyo. “amesema.
Aidha amesema kuwa ,wanaangalia namna ya kufanya maboresho katika masuala ya bima ambapo amesema Posta kwa sasa wanajitahidi sana katika kuhakikisha hawatumii tena barua kama zamani hivyo wanakimbizana kupokea teknolojia ili waweze kutimiza malengo yao .
Naye Katibu Mkuu wa PAPU Afrika,Dkt Sifundo Chifu Moyo amesema kuwa , kuna baadhi ya changamoto ambazo kwa asilimia kubwa tayari viongozi wa nchi hizo wameanza kuzitafutia Ufumbuzi ikiwemo ajenda ya kuendelea kuwasilisha michango kwa kuzingatia mapato kutoka kwa nchi wanachama shabaha kuu ikiwa ni kufikia malengo kwa kutambua umuhimu wa Umoja huo wa posta Afrika.
“Sekta ya posta bado ina mchango mkubwa katika Uchumi na maendeleo kwa kuzingatia masuala ya utawala ikiwemo ajenda ya Kupokea na kuifanyia kazi matumizi ya akili mnemba yaani (Artificial intelligence),katika Hali hiyo ipo haja kwa mataifa haya kuzidi kuimarisha shughuli za kibiashara ili kukuza uchumi wa mataifa haya pamoja na ulipaji Kodi” amesema Posta masta Mkuu Maharage Chande.
Mkutano huo wa 42 wa baraza la Utawala Afrika umewakutanisha Wataalamu mbalimbali kutoka mataifa zaidi ya 15 sambamba na ufunguzi wa Vikao vya Wataalamu wa masuala ya posta kwa maendeleo ya mataifa hayo yanayo unda umoja wa posta barani Afrika.