Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti, akiangalia teknolojia ya vifaa vya kisasa vya ufugaji.
Meneja Ubora wa Shafa Farm,Tumaini Sedia (kulia) akimweleza Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti (kushoto )akiangalia bidhaa ya maziwa inayozalishwa na kampuni ya Shafa Farm kabla ya kufunga maadhimisho ya kitaifa ya wiki ya maziwa jijini Mwanza, leo.
 Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti (kulia) akiteta  jambo na Naibu Katibu Mkuu  wa Wizara hiyo, Profesa Daniel Mushi, alipokagua banda la Kanisa la Kirutheri Tanzania, leo jijini Mwanza.
 Ofisa Ubora na Mtaalam wa Bima (QRMO) wa Mamlaka ya Usiamamizi wa Bima (TIRA),Isango Halfan (kushoto),leo akimpa maelezo Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti (wa pili kulia), namna wanavyowahudumia wafugaji na wakulima kuwapa elimu ya umuhimu wa kukatia bima mazao na mifugo yao, wa kwanza ni Naibu Katibu Mkuu wa Izara hiyo, Profesa Daniel Mushi.  
…………………… 

 BALTAZAR MASHAKA, MWANZA

NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi,Alexander Mnyeti ameigiza Bodi ya Maziwa kuangalia changamoto za sekta ya maziwa zikiwemo zinazokwaza jamii kunywa maziwa hasa ya kipato cha chini na kuzifanyia kazi.

Ameagiz aleo wakati akifunga maadhimisho ya Wiki ya Maziwa yaliyofanyika Kitaifa jijini Mwanza akisema unywaji wa maziwa kwa Watanzania sasa ni anasa  na watoto kutokunywa maziwa wanapata udumamvu sababu bei ya bidhaa hiyo kuwa juu.

“Watanzania kunywa maziwa inaoneakana anasa, kopo dogo la maziwa linauzwa sh.700 haiwezekeni kumpa mtoto akanunue maziwa,zipo familia duni kiasi hicho ni mlo wa siku.Tumewaachia wenye uwezo wanywe pekee yao na kuwakosesha fursa hiyo wasio na uwezo,”amesema Mnyeti.

Amesema TDB ifanyie kazi changamoto hizo Watanzania wanywe maziwa, vinginevyo yatabaki ya kupigia picha sababu ya gharama kubwa huku akiwashauri wasindikaji wa maziwa kutumia vifungashio vya karatasi vinavyotokana na miti kuepuka kutumia mifuko ya nylon (plasitiki).

Naibu Waziri huyo amesema Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amerahisisha ufugaji bora kwa kugawa mbegu za madume bora ya ng’ombe wa kisasa wenye tija, hivyo wafugaji wachangamkie fursa hiyo.

“Rais Dk. Samia pia ameruhusu benki zitoe mikopo kwa wafugaji, changamkieni mikopo hiyo kama wavuvi walivyokopeshwa vizimba.Msilalamike kopeni fedha zipo,hatutaki ng’ombe wa kuzalisha lita  tano za maziwa kwa siku na hatutaki mpeleke mifugo yeni kwenye  mashamba ya wananchi, kopeni mfuge kisasa,”amesema.

Msajili wa Bodi ya Maziwa,Profesa George Msalya amesema kwa miaka ya karibuni wametumia sh.bilioni 23 kuagiza maziwa nje sababu ya mchango mdogo wa tasnia ya maziwa,watazigeuza changamoto kuwa fursa  za kukuza na kuongeza mchango katika uchumi wa nchi.

“Elimu waliyopata wazalishaji na wasindikaji wa maziwa wakaitumie kuongeza mchango katika tasnia kwa kuzalisha maziwa ya unga tuondoe gharama za kuagiza maziwa nje,”amesema.

Mwenyekiti wa Bodi, Profesa Zacharia Masanyiwa amesema wadau watumie maarifa, elimu na ujuzi  waliopata kwa uchumi na maendeleo ya tasnia ya maziwa na kuimarisha uchumi wa kaya nchini.