Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Zanzibar Mhe. Riziki Pembe Juma,akifungua kakao cha Waratibu wa jinsiakatika shehia za Unguja huko Ukumbi wa Kwa wazee Sebleni Wialaya ya Mjini.
Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Siti Abasi Ali wakati alipokuwa akitoa maelezo katika kikao cha Waratibu wa Jinsia, shehia za Unguja huko ukumbi wa kwa Wazee Sebleni Wilaya ya Mjini.
Katibu wa Waratibu jinsia katika Wilaya ya Kati Bibi Bahati Issa Suleiman wakati alipokuwa akichangia katika kikao cha Waratibu wa Jinsia, shehia za Unguja,kikao mbacho kimefanyika huko ukumbi wa kwa Wazee Sebleni Wilaya ya Mjini.
Waratibu wa Jinsia, Shehia za Unguja, wakimsikiliza Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Zanzibar Mhe. Riziki Pembe Juma (hayupo Pichani) huko ukumbi wa kwa Wazee Sebleni Wilaya ya Mjini.
Na Takdir Ali. Maelezo.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Zanzibar Riziki Pembe Juma amesema Serikali inafahamu umuhimu wa Watatibu wa Jinsia katika Shehia na itaendelea kuweka mikakati ya kuwawezesha ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi.
Ameyasema wakati alipokuwa akifunguwa kikao cha Waratibu wa jinsia katika Shehia za Unguja huko katika ukumbi wa kwa Wazee Sebleni Wilaya ya Mjini.
Aidha amewataka kushikamana, kuwatetea, kuwalinda, kuhifadhi na kutafuta haki za Wanawake na Watoto ili kuwaepuka na janga la ukatili na udhalilishaji.
Sambamba na hayo amewataka Waratibu hao, kujikita zaidi kutoa elimu katika jamii na sio kusubiri mpaka matokeo yatokee ndio waanze kuyafanyia kufuatilia.
“Waratibu tunafanya kazi nzuri lakini tujikite zaidi kutoa elimu kwa jamii na sio tusubiri mpaka litokee tukio ndio tuanze kufuatilia, kama tunavyojuwa kinga ni bora kuliko tiba,” Alisema Waziri Pembe.
Amefahamisha kuwa, lengo la kuweka vikao na Masheha ni kuwasisitiza kutoa mashirikiano zaidi na Waratibu hao ili waweke vikao mbalimbali vya kutoa elimu hususan katika Skuli za Maandalizi na Madrasa ili Watoto hao waweze kujitambua.
Kwa uapnde wake Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya jamii, jinsia na Watoto Siti Abasi Ali amesema Idara yake imeweka utaratibu wa kukutana kila baada ya miezi 4 ili kujadili masuala mbalimbali yanayohusu wanawake na Watoto.
Amesema vikao hivyo, vimeweza kuwa chachu ya kuwaunganisha pamoja Waratibu hao na kusaidiana katika kupanga mikakati ya kutoa elimu ili kuwakinga Wanawake na Watoto katika vitendo vya udhalilishaji.
Nao Waratibu hao, wameiomba Serikali kuwatatulia matatizo yanayowakabili ikiwemo utelekezaji wa Wanawake na Watoto, vigenge vya Vijana wahuni na ukosefu wa vitambulisho maalum vya kufanyia kazi ili kuepukana na matatizo yanayojitokeza kwani baadhi yao wamekuwa wakipata mashirikiano madogo kutoka kwa Masheha na Jeshi la Polisi.