Mhandisi wa Ujenzi kutoka ofisi ya meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania(TANROADS)Mkoa wa Ruvuma Irene Wilon Kapinga kulia,akisalimiana na baadhi ya wananchi wa kijiji cha Nalas wilayani Tunduru baada ya kukagua uharibifu wa miundombinu ya barabara ya Mtwarapachani -Tunduru yenye urefu wa kilometa 300 iliyotokana na mvua za El-nino.
Muonekano wa sehemu ya Barabara hiyo ambayo wananchi wanaiomba Serikali kujenga kwa lami ili kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji wa bidhaa hasa mazao kutoka shambani kwenda sokoni.
Na Mwandishi Wetu,
Namtumbo
BAADHI ya wananchi wa kijiji cha Lusewa na Lingusanguse wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma,wameiomba Serikali kuharakisha mchakato wa ujenzi wa Barabara kwa kiwango cha lami kutoka MtwaraPachani hadi Tunduru yenye urefu wa kilometa 300 ili waweze kuondokana na adha wanayopata wanapopita katika Barabara hiyo hasa wakati wa masika.
Wamesema,Barabara hiyo itakapojengwa kwa kwa lami,itaharakisha sana usafiri wanapohitaji kwenda makao makuu ya wilaya Namtumbo mjini au makau makuu ya mkoa Songea kwa ajili ya kufuata huduma mbalimbali ikiwemo za kiserikali.
Abuu Mlanda alisema,ubovu wa barabara inasababisha baadhi ya wagonjwa kufia njiani kabla hawajafika Hospitali ya wilaya au Hospitali ya rufaa Songea kwa ajili ya kupata huduma zaidi za matibabu.
Juma Yasin,ameishukuru TANROADS kwa kufanya ukarabati wa mara kwa mara,lakini ameshauri ni vema barabara hiyo ikajengwa kwa lami ili kuokoa fedha zinazotumika kufanya matengenezo kwa kiwango cha changarawe mwaka hadi mwaka.
Mkazi wa kijiji cha Lingusanguse ambaye ni dereva boda boda Raja Nawenya alisema,nyakati za masika barabara hiyo inapitika kwa shida kutokana na kujaa maji kila sehemu na kusababisha magari kukwama.
Alisema,safari za kwenda makao makuu ya wilaya zinakuwa ngumu na wanatumia muda mrefu hadi kufika kwa kuwa kila mmoja anahofia kutembea mwendo wa haraka kutokana na mashimo mengi yanayohatarisha usalama wao na vyombo vyao.
Kwa upande wake msimamizi wa Barabara hiyo kutoka wakala wa barabara Tanzania(TANROADS)mkoa wa Ruvuma Mhandisi Irene Kapinga,amewahakikishia wananchi wa wilaya ya Namtumbo na Tunduru kuwa, Barabara ya MtwaraPachani-Nalasi itajengwa kwa kiwango cha lami pindi serikali itakapopata fedha.
Kapinga alisema,hakuna shughuli zitakazosimama kutokana na ubovu wa miundombinu,kwani wako kazini na wanaendelea kufanya matengenezo ya dharura na matengenezo ya kawaida kwenye maeneo yote yaliyoharibika na mvua kubwa za El-nino.
Aidha Kapinga,ameishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwapatia fedha ili kufanya matengenezo ya barabara hiyo inayounganisha wilaya ya Namtumbo na Tunduru.
“barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami pindi serikali yetu itakapopata fedha,kwani tayari imeshafanyiwa upembuzi na usanifu,nawaomba sana wananchi kuwa wavumilivu”alisema Kapinga.
Kwa mujibu wa Kapinga,kwa sasa barabara hiyo iko kwenye kiwango cha cha ngarawe na kutokana na umuhimu wake kiuchumi TANRODAS,inafanya matengenezo ya mara kwa mara ili kuruhusu shughuli za usafiri na usafirishaji kufanyika msimu wote wa mwaka.