Na Albano Midelo,Songea
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed ameyafungua rasmi mashindano ya michezo ya UMITASHUMTA na UMISSETA mwaka 2024 kwenye uwanja wa Majimaji mjini Songea.
Akizungumza kabla ya kufungua mashindano hayo ambayo yanashirikisha Halmashauri zote nane,Mkuu wa Mkoa amesema ubora wa wachezaji katika timu nyingi hasa mchezo wa soka wameanzia mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA hatimaye kuchukuliwa na vilabu vikubwa.
Ametolea mfano mashindano ya UMISSETA katika Mkoa wa Ruvuma yamewatengeneza vijana kupitia timu ya soka iliyoshiriki mashindano hayo katika ngazi ya Taifa na Mkoa kuibuka mshindi wa kwanza hivyo kuchukua kikombe cha UMISSETA Taifa mwaka 2019.
“Baadhi ya vijana kutoka Ruvuma hawakuishia hapa,walishiriki mashindano hayo katika ngazi ya Afrika Mashariki,ushiriki wao katika ngazi hizo ulifanya wachezaji kama Nathaniel Chilambo anayechezea timu ya Azam Sports kuibuliwa,Golikipa wa Timu yetu ya UMISSETA Mkoa Nice Kahemela ambaye kwa sasa anachezea Sports Academy iliyopo nchini Afrika ya Kusini ’’,alisema Kanali Abbas.
Mkuu wa Mkoa amewataja wachezaji wengine walioibuliwa kutokana na mashindano ya UMISSETA Ruvuma kuwa ni Neva Kabona kwa sasa yupo Zanzibar anachezea timu ya JKU,kijana mwingine ni Simba Simba ambaye baada ya mashindano hayo alipata ufadhili wa Kwenda kusoma nchini Marekani na John Chikungu ambaye hivi sasa ni mchezaji wa Ruvuma Shooting.
“Nimeona niwataje wachezaji hawa ili mjue kuwa mashindano haya yakitiliwa msukumo unaostahili ni faida kubwa kwa vijana wetu na Taifa letu’’,alisema Mkuu wa Mkoa.
Amebainisha Zaidi kuwa serikali kwa kutambua umuhimu wa michezo,Sanaa na utamaduni imeongeza tasnia ambazo zitakuwa chachu kwa vijana ili kuinua vipaji katika mitaala ya elimu.
Hata hivyo amesisitiza kuwa malengo ya kuinua vipaji vya vijana yatafikiwa iwapo wadau wote wanaohusika na michezo watashirikiana na kufanya kazi kwa Pamoja ambapo amesema serikali imeanza kuimarisha michezo kwa kutenga shule 56 kati ya hizo shule tatu zipo mkoani Ruvuma ambazo ni Songea Boys,Maposeni na Mahanje.
Awali akitoa taarifa ya mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA ,Kaimu Afisa Elimu wa Mkoa wa Ruvuma Mathias Tilia amesema katika mashindano ya mwaka huu jumla ya wanafunzi 658 wanashiriki mashindano ya Mkoa mwaka huu ili kupata wanafunzi 120 ambao watawakilisha Mkoa wa Ruvuma kwenye mashindano ya kitaifa yanayofanyika mkoani Tabora.
Kaulimbiu ya Michezo ya UMITASHUMTA na UMISSETA mwaka huu inasema Tunajivunia mafanikio katika sekta ya elimu,michezo na Sanaa,hima Mtanzania shiriki uchaguzi wa serikali za mitaa 2024.