Na Mwandishi wetu, Dar es salaam
WAANDISHI wa habari 24 wa mikoa ya Manyara, Kilimanjaro na Morogoro, wamejengewa uwezo na mtandao wa jinsia Tanzania (TGNP) juu ya kutokomeza ukatili wa kingono, kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi kwenye kilimo ikolojia kuimarisha uhakika wa chakula.
Mkurugenzi mtendaji wa TGNP, Lillian Liundi akizungumza kwenye mafunzo ya siku tatu yaliyofanyikia ukumbi wa mtandao huo jijini Dar es salaam, amesema mradi huo unahusisha halmashauri ya wilaya ya Mbulu mkoani Manyara, Gairo na Morogoro na Mwanga mkoani Manyara.
Liundi amesema waandishi wa habari kupitia vyombo vyao wana nguvu kubwa katika kuielimisha jamii kwenye ukatili wa kingono, wanawake katika uongozi na kilimo ikolojia.
Amesema waandishi wa habari wanapaswa kuandika habari nyingi zaidi za wanawake katika kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarakia kufanyika mwaka huu wa 2024.
“Wanawake waelimishwe katika kugombea nafasi za uongozi n tusiweke mbele vikwazo ila tutangaze fursa na mafanikio,” amesema Liundi.
Amesema wanawake wakishiriki na kuelewa ipasavyo watapata nafasi kupitia lengo la 50 kwa 50 ili kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi.
Hata hivyo, amesema kilimo ikolojia ni kilimo cha kiafya kisicho na madhara ndiyo sababu serikali imeipa kipaumbele benki ya mbegu za asili.
“Tunahitaji jitihada na juhudi zaidi katika kunyanyua kilimo ikolojia kwani ni kilimo hai na salama,” amesema Liundi.
Mwezeshaji wa TGNP, Catherine Mzurikwao amesema ukatili wa kijinsia umefanyika kwa baadhi ya wanawake wa kata ya Murray wilayani Mbulu mkoani Manyara.
Mzurikwao amesema matukio ya ukatili wa kingono na ukatili umefanyika kwenye msitu wa Nou japokuwa hivi sasa umepungua.
Amesema ulevi wa pombe umechangia matukio ya ukatili kwani kata haina kituo cha polisi na uhalifu ukitokea wahalifu na watuhumiwa hukamatwa kupitia ofisi ya ofisa mtendaji wa kata (WEO).
Mmoja kati ya waandishi wa habari walioshiriki mafunzo hayo ya siku tatu John Walter ameishukuru TGNP kwa kuwapa mafunzo hayo kwani wamejengewa uwezo zaidi katika kutekeleza wajibu wao.
Walter amesema wataandika zaidi matukio ya ukatili wa kingono, wanawake katika uongozi na kilimo ikolojia katika kujadili mtazamo wa kijamii.