Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Elimu) Dkt. Charles Msonde akizungumza na Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule, Walimu Wakuu na Walimu waliopo Halmashauri za Wilaya ya Biharamulo (hawapo pichani) wakati wa kikao kazi chake na maafisa hao.
Sehemu ya Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule, Walimu Wakuu na Walimu waliopo Halmashauri za Wilaya ya Biharamulo wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Elimu) Dkt. Charles Msonde (hayupo pichani) wakati wa kikao kazi chao na Naibu Katibu Mkuu huyo.
Baadhi ya Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule, Walimu Wakuu na Walimu waliopo Halmashauri za Wilaya ya Biharamulo wakiwa katika kikao kazi na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Elimu) Dkt. Charles Msonde (hayupo pichani).
Baadhi ya Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule, Walimu Wakuu na Walimu wa Halmashauri za Wilaya ya Biharamulo wakimsikiliza kwa makini Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Elimu) Dkt. Charles Msonde (hayupo pichani) wakati wa kikao kazi chao na Naibu Katibu Mkuu huyo.
Na. James Mwanamyoto, OR-TAMISEMI
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Elimu) Dkt. Charles Msonde amewataka walimu wenye madai ya malimbikizo ya mishahara (arrears) kuwasilisha vielelezo vya madai yao kwa Maafisa Elimu ili wayashughulikie, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa anayetaka changamoto zote za walimu zitatuliwe.
Dkt. Msonde ametoa wito huo kwa nyakati tofauti, wakati wa vikao kazi vyake na Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule, Walimu Wakuu na Walimu waliopo katika Halmashauri za Wilaya ya Biharamulo na Muleba.
“Walimu kuanzia sasa wasilisheni madai yenu na viambata vyake muhimu kwa Maafisa Elimu ili wao ndio wawasilishe kwa Maafisa Utumishi kwa ajili ya kushughulikiwa, na kuongeza kuwa waziri mwenye dhamana Mhe. Mohamed Mchengerwa alishaelekeza madai yote ya walimu yashughulikiwe,” Dkt. Msonde amesisitiza.
Dkt. Msonde amesema, Maafisa Elimu watekeleze jukumu hilo kwani wapo kwa ajili ya kuwahudumia walimu hivyo ni wajibu wao kuwafuata Maafisa Utumishi Wakuu ili kushirikiana nao katika kushughulikia madai ya malimbikizo ya walimu.
Dkt. Msonde amehimiza kuwa, Afisa Elimu akishawasilisha madai ya malimbikizo ya mishahara ya watumishi kwa Afisa Utumishi Mkuu anapaswa pia kuwapatia mrejesho watumishi husika ili wajue ni hatua ipi imefikiwa katika kushughulikia madai yao.
“Afisa Elimu iwapo ukienda kwa Afisa Utumishi na asikupe ushirikiano, nenda kwa Mkurugenzi wa Halmashauri na unijulishe mimi ili tuchukue hatua stahiki kwa Afisa Utumishi huyo ambaye anakaidi maelekezo halali ya waziri mwenye dhamana Mhe. Mohamed Mchengerwa,” Dkt. Msonde amesisitiza.
Dkt. Msonde amehitimisha siku ya kwanza ya ziara yake mkoani Kagera kwa kuhimiza uwajibikaji kwa Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule, Walimu Wakuu na Walimu waliopo Halmashauri za Wilaya ya Biharamulo na Muleba.