Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Kailima, R. K akizungumza na waandishi wa habari mkoani Kigoma leo tarehe 29 Mei, 2024.
Na Mwandushi wetu, Kigoma
Wapiga kura wapya 224,355
wanatarajiwa kuandikishwa mkoani Kigoma wakati wa uboreshaji wa Daftari la
Kudumu la Wapiga Kura unaotarajiwa kufanyika mkoani humo kwa siku saba kuanzia
tarehe 01 hadi 07 Julai, 2024.
Uboreshaji huo wa Daftari
utatanguliwa na uzinduzi wa zoezi hilo utakaofanyika tarehe 01 Julai, 2024
mkoani Kigoma ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.
Akizungumza na waandishi wa
habari mkoani Kigoma leo tarehe 29 Mei, 2024, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume
Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Kailima, R. K amesema wapiga kura hao ni
ongezeko la asilimia 21.50 ya wapiga kura 1,043,281 waliopo kwenye Daftari
mkoani Kigoma.
“Kwa Mkoa wa Kigoma ambao una
Halmashauri ya Manispaa moja, Halmashauri ya Mji moja na Halmashauri za Wilaya
sita, majimbo ya uchaguzi nane na kata 488, Tume inatarajia kuandikisha wapiga
kura wapya 224,355. Hii ikiwa ni ongezeko la asilimia 21.50 ya wapiga kura
1,043,281 waliopo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Hivyo, Tume
inatarajia baada ya uandikishaji, Mkoa wa Kigoma utakuwa na wapiga kura
1,267,636,” amesema Bw. Kailima.
Akizungumzia makadirio ya
wapiga kura wapya watakaoandikishwa nchi nzima, Bw. Kailima amesema Tume
itaandikisha wapiga kura wapya 5,586,433 sawa na asilimia 18.7 ya wapiga kura
29,754,699 waliopo kwenye Daftari baada ya uboreshaji uliofanyika mwaka
2019/20.
“Katika zoezi hili,
inatarajiwa wapiga kura 4,369,531 wataboresha taarifa zao na wapiga kura
594,494 inatarajiwa wataondolewa kwenye Daftari kwa kukosa sifa za kuendelea
kuwepo kwenye Daftari. Hivyo, baada ya uboreshaji, inatarajiwa kuwa Daftari
litakuwa na jumla ya wapiga 34,746,638,” amesema Bw. Kailima.
Kuhusu idadi ya vituo vya
kuandikisha wapiga kura, Bw. Kailima amesema katika uboreshaji wa Daftari la
Kudumu la Wapiga Kura mwaka huu wa 2024 kutakuwa na jumla ya vituo 40,126,
ambapo kati ya vituo hivyo, 39,709 ni vya Tanzania Bara na vituo 417 ni vya Zanzibar.
“Vituo hivi ni ongezeko la
vituo 2,312 ikilinganishwa na vituo 37,814 vilivyotumika kuandikisha wapiga
kura mwaka 2019/2020,” amesema.
Mkurugenzi huyo wa Uchaguzi
amesema kwa Mkoa wa Kigoma vituo 1,162 vitatumika kwenye uboreshaji wa mwaka
huu ikiwa ni ongezeko la vituo 69 katika vituo 1,093 vilivyotumika kwenye
uboreshaji mwaka 2019/20.
Zoezi hili la uboreshaji
litahusisha kuandikisha wapiga kura wapya ambao ni raia wa Tanzania wenye umri
wa miaka 18 na zaidi na watakaotimiza umri huo ifikapo tarehe ya uchaguzi mkuu
wa mwaka 2025 pamoja na wale ambao hawajapoteza sifa za kuendelea kuwemo kwenye
Daftari kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi au sheria nyingine yeyote.
Uboreshaji pia utahusu kutoa
fursa kwa wapiga kura walioandikishwa awali na ambao wamehama kutoka mkoa au
wilaya moja kwenda nyingine waweze kuhamisha taarifa zao kutoka kata au jimbo
walioandikishwa awali.
Zoezi hilo pia litatoa fursa
kwa wapiga kura walioandikishwa kurekebisha taarifa zao yakiwemo majina na
taarifa nyingine, kutoa kadi mpya kwa wapiga kura waliopoteza kadi au kadi
kuharibika na kuondoa wapiga kura waliopoteza sifa za kuwemo kwenye Daftari
kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuukana uraia wa Tanzania na
kifo.