Na.Alex Sonna-TANGA
Chuo Cha Takwimu Mashariki mwa Afrika (EASTC), kinashiriki maonesho ya kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu 2024 yaliyoanza tarehe 25 hadi 31 Mei, 2024 jijini Tanga.
Maonesho hayo yenye lengo la kukuza ubunifu na sekta ya elimu nchini kwa mwaka huu yameambata na kauli mbiu ya “Elimu, Ujuzi, Ubunifu na Teknolojia kichocheo cha Maendeleo kwa Uchumi Shindani.”
Sambamba na maonesho haya dirisha la maombi ya kujiunga na vyuo vya elimu ya juu limefunguliwa kwa wanafunzi wa ngazi ya Astashahada, Stashahada, katika masomo mbalimbali.
Makamu Mkuu wa Chuo Mipango,Fedha na Utawala Dkt France Shayo amewataka wahitimu wa Sekondari na waombaji wengine wanahitaji kujiunga na masomo katika chuo hicho kwa ngazi ya Astashahada na Stashahada kutumia fursa hii kusajili katika kipindi hiki cha maonesho kwenye Banda la Chuo hicho katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Popatlal kuanzia Mei 25 hadi Mei 31, 2024 .
Amesema wananchi wanayo fursa ya kufanya udahili wa hapo kwa hapo kwa njia ya mtandao (online registration) katika banda la Cha Takwimu Mashariki mwa Afrika (EASTC) katika maonesho ya wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu au kufika katika Kampasi za chuo mkoani Dodoma au Dar es salaam kwa ajili ya mwaka wa masomo 2024/2025 utakaoanza Oktoba mwaka huu.
Mkuu wa Idara ya Mawasiliano na Masoko Bw. Samwel Marandu ameongeza kuwa mwanafunzi anaweza kufanya usajili kwa njia ya mtandao popote pale alipo kwa kutembelea tovuti ya chuo ya www.eastc.ac kwa taarifa zaidi kuhusu kozi na taratibu zingine za kujiunga.
Maafisa kutoka Idara ya Mawasiliano na Masoko wa chuo hicho wanaendelea kutoa elimu kuhusu masuala ya kitaaluma ikiwemo udahili wa wanafunzi waliomaliza kidato cha nne na kidato cha sita kwa wanafunzi na watu mbalimbali wanaofika na kutembelea Banda la Cha Takwimu Mashariki mwa Afrika (EASTC) katika Maadhimisho hayo.
Wananchi mbalimbali pamoja na wanafunzi waliomaliza kidato cha nne na cha sita wanakaribishwa kupata elimu pamoja na kufanya udahili ambao unafanywa bure kabisa bila malipo yoyote.
“Wanawakaribisha wananchi kutembelea banda la Chuo hicho kwani timu nzima ya masoko ipo tayari kuwahudumia na kutoa elimu kwa undani zaidi kuhusu kozi mbalimbali zinazotolewa na chuo hicho alisema Bw.Marandu.
Chuo pia kinaonesha ubunifu wa mmoja wanafunzi wa mwaka wa pili, Bw. Emmanuel Mgonda, anayeendelea na masomo ya shahada ya Sayansi ya Takwimu katika chuo hicho Kampasi ya Dar es Salaam aliyebuni Mfumo wa tehema utakaotumika kwenye bwawa la kufugia samaki.
Maadhimisho haya yanawapa fursa wananchi kujifunza mfumo wa “Automated Fish Pond” unasaidia wananchi hususani wafugaji wa samaki kupunguza gharama za ufugaji na usimamizi wa mabwawa ya samaki.
Aidha,Bw.Mgonda ameelezea mfumo huo unaoendeshwa kwa kutumia tehama unasaidia kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya mazingira au hali ya maji yasiyo rafiki katika ufugaji wa samaki.