Na Mwandishi wetu, Haydom
MASHINDANO ya mbio za Haydom marathon 2024 yamekusanya Sh100 milioni kwa ajili ya fedha za kuongeza vitanda vya wodi ya mama na watoto kwenye hospitali ya rufaa ya kilutheri ya Haydom Wilayani Mbulu Mkoani Manyara.
Mkurugenzi wa hospitali hiyo Dk Pascal Mdoe akizungumza kwenye mbio za Haydom marathon 2024, amesema lengo lilikuwa kukusanya kiasi cha Sh130 milioni kwenye mashindano hayo kwa ajili ya kuongeza vitanda vingine.
Dk Mdoe amesema wamelenga kununua vitanda 200 ambavyo vitaongezwa kwenye wodi ya mama na mtoto katika hospitali hiyo.
“Tunatarajia kukamilisha kiasi hicho kilichobakia cha Sh30 milioni kwani tunaendelea kukusanya na pia wenzetu wa Norway watakimbia pia kutuunga mkono wa kupata fedha hizo,” amesema Dk Mdoe.
Akizungumzia juu ya mashindano hayo amesema kwa mwaka huu wametenga Sh5 milioni kwa ajili ya zawadi kwa washindi, ila mwezi Mei mwaka 2025 watatenga Sh10 milioni.
Mbunge wa jimbo la Mbulu Vijijini Flatei Gregory Massay ambaye ameshiriki mbio za Haydom marathon kilomita mbili amewapongeza viongozi wa hospitali hiyo kwa kuandaa mashindano hayo ili kununua vitanda vingine vya wodi ya mama na mtoto.
“Mimi binafsi nachangia Sh1 milioni siyo fedha za mfuko wa jimbo ni zangu binafsi, kwenye kazi hii ya ununuzi wa vitanda katika wodi ya mama na watoto kwenye hospitali ya rufaa ya Haydom,” amesema Massay.
Amewapongeza viongozi, madaktari na wauguzi wa hospitali hiyo kwa namna wanavyotoa huduma ya matibabu kwa jamii.
Mshindi wa kwanza kwenye mbio za Haydom marathon kilomita 21 Mao Ako kutoka Katesh wilayani Hanang’ amesema mashindano yalikuwa magumu ila anamshukuru Mungu ameshinda nafasi hiyo..
Ako amesema lengo lake lilikuwa kushinda mashindano hayo na ameweza ila atongeza juhudi katika mashindano ya riadha ili aweze kuwa mbele zaidi.
Mmoja kati ya wakazi wa kijiji cha Getanyamba, Yasinta Hamay amesema hospitali ya rufaa ya Haydom imekuwa mkombozi kwa wanawake na watoto wa eneo hilo hivyo wanawapongeza kwa ubunifu huo.
“Vitanda vingine vikiongezwa katika wodi ya mama na mtoto itakuwa vyema mno kwani huduma zitakuwa bora zaidi ya ilivyo,” amesema.