Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed akizungumza kwenye ufunguzi wa masoko ya ufuta,soya na mbaazi kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani na TMX
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed akiwaongoza wakazi wa Mji wa Namtumbo kwenye ufunguzi wa masoko ya ufuta,soya na mbaazi kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani na TMX
Na Albano Midelo,Namtumbo
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed amefungua masoko ya ufuta,soya na mbaazi kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani na TMX wilayani Namtumbo.
Katika uzinduzi wa mnada wa kwanza mkoani Ruvuma katika zao la ufuta jumla ya kilo milioni 1,293,000 umeuzwa kwa bei ya wastani wa shilingi 3,903 kwa kilo.
Akizungumza kwenye ufunguzi huo,Kanali Abbas amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mfumo mzuri wa masoko ya mazao ya wakulima ambapo amesema mfumo huo unaleta manufaa makubwa kwa wakulima.
Amebainisha kuwa ,uendeshaji wa masoko ya zao la ufuta,mbaazi na soya hufanyika kupitia wakulima kununua,kusafirisha na kukusanya mazao kwenye vyama vya msingi 101 vilivyopo katika wilaya za Namtumbo,Songea,Mbinga,Nyasa na Tunduru na vyama vikuu vya ushirika viwili ambavyo ni TAMCU na SONAMCU.
“Mfumo wa stakabadhi ghalani umedhibiti vipimo visivyo halali ambavyo vinamuibia mkulima kwa kuwa mfumo unatumia mizani ya kidijitali ambapo taarifa zote zinakuwa zimehifadhiwa’’,alisema.
Hata hivyo amekemea suala la utoroshaji wa mazao ambapo ameagiza serikali za mitaa kudhibiti vitendo vya utoroshaji wa mazao na kuziagiza Halmashauri zihakikishe minada inaanza mapema kwa kuzingatia ratiba na kuweka usimamizi Madhubuti wa vyama vya ushirika katika shughuli zote zinazohusu mifumo ya masoko.
Mkuu wa Mkoa ameziagiza Halmashauri kuhakikisha zinatoa elimu ya mifumo ya masoko kwa wakulima na wadau wengine ambapo pia amewataka wanunuzi wa mazao na vyama vikuu vya ushirika kuhakikisha wanafanya malipo yab wakulima kwa wakati.
Naye Meneja Mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Wilaya za Songe ana Namtumbo (SONAMCU) Juma Mwanga ameyataja hali ya masoko kwa mazao ya ufuta,soya na mbaazi inaridhisha ambapo katika kipindi cha miaka minne katika zao la ufuta jumla ya kilo 22,974,950 ziliuzwa na kuingiza Zaidi ya shilingi bilioni 59.
Amesema zao la soya katika kipindi cha miaka minne zimeuzwa kilo 12,915,722 na kuingiza Zaidi ya shilingi bilioni 13 na zao la mbaazi katika kipindi hicho zimeuzwa kilo 13,415,316 ambazo zimeingiza Zaidi ya shilingi bilioni 16.
Ameyataja baadhi ya mafanikio ya mazao mchanganyika yaliyouzwa kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani kuwa ni wakulima kupata bei nzuri ya mazao,kupungua kwa kiwango cha utoroshaji wa mazao,kuongezeka kwa wanunuzi na kuwepo ushirikiano baina ya wadau wa stakabadhi ghalani kuanzia ngazi ya Kata hadi Mkoa.