Na Gideon Gregory, Dodoma.
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imeweka bayana mafanikio ya Taasisi hiyo katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkoa wa Dodoma na kuongeza kuwa TFS imeendelea kutekeleza usimamizi na ulinzi wa Hifadhi za misitu sambamba na utekelezaji wa maagizo yaliyopo kwenye ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020/2025.
Hayo yameelezwa na Meneja Msaidizi, Kitengo cha Rasilimali Misitu Bi.Husna Msagati mbele ya waandishi wa Habari wakati wa kipindi maalum cha Mitatu Dodoma na Samia kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dodoma.
Bi. Msagati amesema Serikali ya awamu ya sita imefanikisha ongezeko la maeneo ya kufugia nyuki, upandaji wa miti kukijanisha Dodoma, ongezeko la watalii Kolo – Kondoa, kuimarika kwa usimamizi wa misitu, uandaaji wa mpango wa matumizi bora ya ardhi .
Ameongeza kuwa mafanikio mengine ni pamoja na kumaliza mgogoro sugu wa mipaka kwa kufanya mapitio ya mipaka ya hifadhi ya msitu, kuweka alama za mipaka zinazoonekana na za kudumu, mabango pamoja na kusafisha mipaka ili kutenga hifadhi na maeneo ya wananchi.
“TFS imeendelea kutatua migogoro kati ya hifadhi za misitu na jamii ambapo eneo lenye Hekta 2,620.3 limemegwa na kurudishwa kwa wananchi katika hifadhi za Mlali kwenye Wilaya ya Kongwa na Kijiji cha Chenene na Mayamaya kwenye Wilaya ya Bahi na hii ni moja ya utekelezaji wa maelekezo ya BLM” Amesema Bi. Msagati.