Na Zillipa Joseph, Katavi
Mkoa wa Katavi ni mojawapo kati ya mikoa 31 ya nchini Tanzania unaopatikana Magharibi mwa nchi hiyo. Ulianzishwa rasmi mnamo Machi 2012 kwa kumegwa kutoka katika mkoa wa Rukwa. Mkoa wa Katavi umepakana na mikoa ya Tabora, Rukwa na Kigoma. Katika sensa ya mwaka 2022 idadi ya wakazi wa mkoa huo ilifikia watu 1,152,958 ambao nusu yake ni watoto.
Kabila kubwa la asili katika mkoa wa Katavi ni Wafipa; lakini pia kuna Wabende, Wapimbwe na Wakonongo. Hata hivyo miaka ya hivi karibuni kumekuwa na makabila mengi yanayohamia mkoani humo hasa Wasukuma kutoka kanda ya ziwa Viktoria.
Wakazi wa mkoa huu wanategemea zaidi shughuli za kilimo, japo pia kuna ufugaji, uchimbaji wa madini na biashara.
Kwa mujibu wa sera ya afya ya Juni mwaka 2007, kipengele namba 5.1 (a) Mkakati wa Afya ya msingi ulilenga kuimarisha afya za wananchi kuanzia ngazi ya kaya, hadi taifa kwa kuwashirikisha wananchi wenyewe.
Mkakati huu ulilenga kuwezesha upatikanaji wa huduma muhimu za afya kwa wananchi wote na ulitoa kipaumbele katika uboreshaji afya, kinga na tiba. Maeneo yaliyozingatiwa katika uboreshaji wa afya ni elimu ya afya, uhamasishaji wa lishe bora, afya ya mazingira na afya mashuleni.
Mkakati huu unafafanua kuwa kinga ni huduma za mama na mtoto, chanjo dhidi ya magonjwa ya kuambukiza na tiba ni matibabu kwa maadili ya kawaida na majeraha, dawa muhimu, huduma ya afya ya akili, kinywa na macho.
Tanzania inaelezwa kuwa nchi mojawapo duniani ambayo ilitekeleza huduma za afya ya msingi kwa mafanikio makubwa sana baada ya uhuru.
Katika kuboresha huduma za afya serikali imekuwa ikitoa chanjo aina mbalimbali kwa ajili ya watoto kuanzia umri wa miaka sifuri hadi miaka nane dhidi ya magonjwa mbalimbali kwa vipindi tofauti tofauti.
Chanjo hizo zimekuwa zikitolewa katika vituo vya kutolea huduma za afya na nyingine zikitolewa katika makazi ya watu kupitia kampeni ya utoaji chanjo ya nyumba kwa nyumba.
Wakazi wa mkoa wa Katavi nao wamekuwa wakinufaika na chanjo hizi. Wamekuwa wakijitokeza kupeleka watoto wao kupata chanjo mara wasikiapo matangazo na wakati mwingine kufuata ratiba za chanjo kwa mujibu wa umri watoto wao katika maudhurio ya kliniki za mama na mtoto.
Katika chanjo ya surua na rubella iliyofanyika mwezi wa pili mwaka huu mkoa ulitarajia kuchanja jumla ya watoto 171,965 wa umri wa kuanzia miezi tisa hadi miaka mitano na walichanja jumla ya watoto 196,957 sawa na asilimia 115%.
Kwenye chanjo ya Polio II iliyofanyika mwezi wa tisa mwaka 2023 ambayo ilikuwa ni chanjo iliyotolewa nyumba kwa nyumba walitarajia kuchanja watoto 225,342 wa umri wa miaka sifuri hadi nane na matokeo yake walichanja jumla ya watoto 445, 551!
Mratibu wa chanjo mkoa wa Katavi Stephan Kahindi amesema mafanikio hayo yanatokana na hamasa kubwa wanayofanya katika kuelimisha jamii umuhimu wa afya.
Baadhi ya kinamama wenye watoto ambao walipata chanjo walisema wanatambua umuhimu wa afya za watoto wao na adha ya kuuguza.
Waliongeza kuwa ni vibaya sana endapo utajikuta unamuuguza mtoto magonjwa ambayo yangeweza kuzuilika kwa chanjo.
Dokta Alex Mrema ni Mganga Mkuu wa wilaya ya Tanganyika, anasema watoa huduma za afya ngazi ya jamii wana mchango mkubwa katika zoezi zima la chanjo.
Watoa huduma ngazi ya jamii wamekuwa wakisaidia hasa katika kampeni ya kutoa chanjo nyumba kwa nyumba kwani wamekuwa wakifika hata katika maeneo yaliyo pembezoni mwa mji.
Filbert Chundu ni Mratibu wa asasi isiyo ya kiserikali ya LARDEO yenye makao yake makuu katika manispaa ya Mpanda. Asasi hiyo inahusika na utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto mkoani Katavi.
Kwa kushirikiana na ofisi ya Katibu Tawala mkoa wa Katavi LARDEO imekuwa ikitoa elimu kwa jamii juu ya kushiriki katika kuwapeleka watoto kupata chanjo.
“Chanjo ni muhimu sana kwa watoto, inasaidia kuwakinga na maradhi mbalimbali. Tazama watoto walivyopata shida kata ya Maji Moto mwaka juzi kwa kuugua surua” alisema Chundu.
Chundu aliitaka jamii kuendelea kuwa mtizamo chanya kwa chanjo dhidi ya magonjwa mbalimbali na kuwapeleka watoto kliniki ili wakapate chanjo kwa mujibu wa ratiba na umri wao.
Mkuu wa mkoa wa Katavi Bi. Mwanamvua Mrindoko ni mmoja wa viongozi aliyeshiriki kwa kiasi kikubwa katika kuhamasisha jamii kuwatoa watoto wao wapate chanjo.
Anakiri kuwa ushiriki wa kinababa katika kuwapeleka watoto kupata chanjo umekuwa ni mdogo kutokana na ukweli kwamba walezi wakuu wa watoto ni kinamama.
Mkuu huyo wa mkoa wa Katavi anatoa wito kwa jamii kuendelea kuwapeleka watoto kupata chanjo katika kliniki na vituo vya kutolea huduma ya afya.
“Chanjo hizi zimeanza miaka mingi. Tuliozaliwa miaka ya nyuma hakuna asiye na alama begani mwake, hiyo ni alama kuwa hata wewe ulipokuwa mtoto ulipata chanjo” alisema Mrindoko katika moja ya kikao kazi na wadau wa malezi na makuzi ya watoto.
Aidha aliwataka wadau wa mashirika mbalimbali yasiyo ya kiserikali kuendelea kuhamasisha jamii umuhimu wa chanjo kwa watoto.
Chanjo ambazo hutolewa kwa watoto ni pamoja na chanjo ya homa ya ini, tetenasi, surua, polio, kifua kikuu, dondakoo, kifaduro, nimonia, surua na rubella.
Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwezi Machi mwaka 2021 zinaonyesha kuwa asilimia 85 ya watoto wa bara la Afrika wanapata chanjo.
Kongole kwa wakazi wa Katavi kwa kuendelea kuitikia wito wa kuwapeleka watoto wakapate chanjo na hivyo kuwakinga dhdi ya magonjwa mbalimbali.