*Na Mwandishi wetu;-
Mbunge wa Jimbo la Babati na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Daniel Sillo ametoa magunia 10 ya mahindi ya chakula kwa waathirika wa mafuriko waliopo katika Kijiji cha Manyara.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi chakula hicho Mei 19, 2024 katika Ziara Maalum ya Kikazi ya kutembelea na kukagua uharibifu wa mali uliotokana na vyanzo mbalimbali vya Ziwa Manyara kuzidiwa na mvua zinazoendelea kunyesha, amewataka Wananchi kupokea kiasi cha chakula kilichopatikana huku Serikali ikiendelea kufanya jitihada nyingine.
“Ndugu zangu nipende kutoa pole kwa wahanga wa mafuriko kwani ni muda sasa wa kutumia chakula kilichokabidhiwa huku Serikali ikiendelea kufanya jitihada mbalimbali ili mpate nafuu pia nionye tabia inayofanywa na makundi ya watu wasio na nia njema kwa kufanya udokozi kwani Vyombo vya Ulinzi na Usalama vipo kazini”Alisema.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Manyara Ndg. Juma Jorojik alisema takribani wakazi 600 hawana pa kuishi wala chakula kwa kuwa mashamba yao pia yamefunikwa na maji yakiwa na mazao mbalimbali.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati Bi. Anna Mbogo amewaagiza wataalamu kuendelea kufanya tathmini ya maafa hayo na kumtaka Mganga Mkuu wa Halmashauri kuhakikisha wanachukua tahadhari kwa Wananchi kuepuka magonjwa ya milipuko.
Hata hivyo, baadhi ya Wananchi wa Kijiji cha Manyara wameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa bega kwa bega katika kipindi kigumu, pia wameomba Serikali kuendelea kupeleka msaada zaidi hasa wa vyakula kutokana na mazao yao kusombwa na maji.