Meneja wa mamlaka ya maji na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) Mkoani Manyara, mhandisi Walter Kirita akisoma taarifa ya utendaji kazi mjini Babati.
Na Mwandishi wetu, Babati
HALI ya upatikanaji maji kwa jamii vijijini Mkoani Manyara hivi sasa imefikia asilimia 70.5 tofauti na asilimia 55.5 mwaka 2019 wakati Mamlaka ya maji na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) ilipoanzishwa.
Meneja wa RUWASA Mkoa wa Manyara mhandisi Walter Kirita akizungumza mjini Babati wakati akisoma taarifa ya kikao kazi amesema hivi sasa wamepiga hatua kubwa ya hali ya upatikanaji wa maji vijijini.
Mhandisi Kirita amesema kwenye mkoa wa Manyara hivi sasa upatikanaji maji umefikia asilimia 70.5 tofauti na RUWASA ilipoanzishwa mwaka 2019 upatikanaji maji uilikuwa asilimia 55.5.
Amesema kuna miradi bado inafanyiwa kazi na wanatarajia ifikapo Desemba mwaka 2024 upatikanaji wa maji utaongezeka kwenye vijiji mbalimbali na kuzidi kupiga hatua kubwa.
“Kila tunachokifanya tunawashirikisha viongozi na wadau siyo kwamba tumemaliza matatizo yote ila tunakuwa kama timu moja katika kufanya kazi,” amesema mhandisi Kirita.
Amesema RUWASA ilianzishwa mwaka 2019 na ilikuta changamoto nyingi ya kutokamilika kwa miradi ya maji iliyokuwa inasimamiwa na halmashauri za wilaya mbalimbali.
Hata hivyo, amesema ili kuwatambua watumishi wa RUWASA waliostaafu, wamewaandalia zawadi kwa ajili ya kutambua mchango wao wakati wakiwa kazini na wabaki na kumbukumbu.
“Stahiki zao za utumishi walikuwa wanapata ila tutawapa zawadi ndogo wakiweka nyumbani wanakumbuka RUWASA na vyeti vya pongezi ili kutambua mchango wao,” amesema mhandisi Kirita.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Cuthbert Sendiga amesema RUWASA wanafanya kazi zao kwa asilimia 100 hivyo wanawapongeza mno kwa wanazozifanya.
“Siyo kwamba hakuna changamoto ya maji Manyara, hapana zipo ila RUWASA ni miongoni mwa taasisi za serikali zinazowajibika kwa jamii ipasavyo hivyo wanastahili sifa,” amesema Sendiga.
Mkazi wa kijiji cha Gabadaw, wilayani Babati, Magdalena Ombay amesema hivi sasa changamoto ya maji imepungua tofauti na awali.
“Hii dhana ya kumtua mama ndoo kichwani imedhihirika huku kwetu kwani baada ya kujitwika ndoo umbali mfupi wanafika nyumbani haraka na kuendelea na shughuli nyingine za kujijenga kiuchumi,” amesema.