Na. Mwandishi wetu – Arusha
Wadau wa masuala ya Utalii wamekutana huko katika Wilaya ya Longido Mkoani Arusha kujadili namna bora ya kukabiliana na tatizo la Wanyamapori kugongwa na magari barabarani na kupelekea wengi kufa.
Mkurugenzi wa Shirika la OIKOS Afrika Mashariki Bi. Mary Birdi amebainisha kuwa kupitia utafiti walioufanya walibaini kuwa Wanyamapori wengi wanafariki kwa kugongwa na magari barabarani hususani katika barabara ya Arusha Namanga.
Ameendelea kufafanua kuwa baada ya kubaini hivyo, wakaona ni vyema kuaandaa semina ambayo itawakutanisha wadau mbalimbali kutoka Serikalini pamoja na Sekta binafsi kujadiliana na kuweka mikakati ya pamoja ya kuona namna bora ya kukabiliana na tatizo hilo ambali linaathiri ikolojia ya Wanyama.
Halikadhalika amebainisha kuwa kupitia semina hiyo ya siku tatu ni imani yake kuwa watakuja na mikakati ya pamoja ya nini kifanyike ili kunusuru ama kupunguza madhara zaidi kutokea dhidi ya Wanyamapori.
Naye Afisa Wanyamapori Mkuu toka Wizara ya Maliasili na Utalii Bwana Issack Ngowi amesema kwa kuzingatia Viongozi Wakuu wa Kitaifa wamekua wakionesha juhudi za kuutangaza utalii wetu, wao watahakikisha wanalinda na kusimamia wanyama hao kuwaepusha na vitendo vya kihalifu ikiwemo ujangili ili Watalii wakifika waone uhalisia wa kile ambacho wamekua wakitangaziwa.
Pia ametoa wito kwa Wananchi kuhakikisha wanakua wazalendo na Nchi yao kwa kutoa taarifa za baadhi ya watu wachache wanaojihusisha na uhalifu dhidi ya wanyamapori ili hatua za Kisheria zichukuliwe dhidi yao.
Kwa upande wake Mkuu wa Polisi Wilaya ya Longido Mrakibu Mwandamizi wa Polisi SSP Leah Ncheyeki amesema kwa kushirikia na wadau wengine watafunga kamera za usalama barabara yote ya Namanga Arusha kwa ajili ya kufuatilia mienendo ya uendeshaji wa madereva katika barabara hiyo.
Aidha amebainisha kuwa Jeshi hilo limejipanga vyema kuhakikisha linasimamia sheria za usalama barabarani kwa kuchukua hatua kwa baadhi ya Madereva watakaobainika kukiuka sheria hizo.
Naye Mkuu wa Ikolojia ya Wanyamapori Kanda ya Longido – Ziwa Natron Bwana Augustino Ngimilanga amesema ili kuhakikisha wanalinda Wanyama hao, watatoa elimu kwa wananchi hasa madereva wa magari juu ya madhara ya kugonga wanyama lakini pia kuwaeleza faida ipatikanayo na wanyama hao kupitia utalii.
Nao baadhi ya madereva wa magari pamoja na kushukuru elimu waliyoipata, wamekiri kuwa kwa kiasi kikubwa wao ndio wanasababisha vifo vingi vya wanyama kwa kutozingatia sheria za usalama barabarani.
Aidha wametoa wito kwa madereva wenzao kuhakikisha wanafuata sheria za usalama barabarani huku wakiomba Wakala wa Barabarani TANROAD kufyeka majani marefu pembezoni mwa barabara kwakua yanachangia kugongwa kwa wanya.