Kaimu Mkurugenzi idara ya udhibiti usalama wa chakula Khadija Ali Sheha akitoa taarifa kwa umma kuhusiana na kusitisha matumizi na kuyaondoshwa sokoni bidhaa maziwa ya kopo ya watoto aina ya INFACARE 1, 2 na 3 kutokana na uwepo wa maneno yanayosomeka hairuhusiwi kuuzwa tena Tanzania “NOT FOR RESALE IN TANZANIA” juu ya makopo ya bidhaa hiyo,hafla iliyo ZFDA Mombasa Zanzibar
PICHA NA FAUZIA MUSSA -MAELEZO ZANZIBAR
Na Fauzi Mussa , Maelezo. Mei 10,2024
Wakala wa Chakula, Dawa na Vipodozi Zanzibar ZFDA imepiga marufuku uingizwaji,uuzwaji, na usamabazaji wa maziwa ya kopo aina ya INFACARE kutokana na kuwepo maandishi yanayokataza kuuzwa nchini kwenye bidhaa hiyo.
Akitoa Taarifa kwa vyombo vya habari kuhusiana na kusitisha matumizi na kuiondosha sokoni bidhaa hiyo huko ofisini kwake Mombasa Zanzibar Kaimu Mkurugenzi idara ya udhibiti usalama wa chakula Khadija Ali Sheha amesema hatua hiyo inalenga kulinda afya za watoto na jamii kwa ujumla.
Ameeleza kuwa kuna baadhi ya wafanyabiashara wanafanya udanganyifu wa kuchuna maandishi hayo na kubandika stika juu ya maandishi au kubadilisha mifuniko halisi ili kuuza bidhaa hiyo, jambo alilosema ni kosa kisheria .
Alifahamisha kuwa hatua mbalimbali za kisheria zitaendelea kuchukuliwa kwa walioghushi na kuingiza nchini bidhaa hiyo kinyume na taratibu zilizowekwa na ZFDA.
Bi Khadija amesisitiza kuwa wataendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kubaini wafanyabiashara wababaishaji na kuwachukuliwa hatua za kisheria watakaobainika kuwa na makosa.
Aidha amesema ZFDA imesitisha matumizi ya maziwa hayo kutokanana kutokukidhi matakwa ya sheria na vigezo vya bidhaa za chakula, kutokusajaliwa na kutothibitishwa kwa ubora na usalama na wakala wa dawa, chakula na vipodozi.
Ameyataja maziwa yaliozuiliwa kuwa ni INFACARE 1,2 na 3 ambayo yapo kwa nambari tofauti za mkupuo na tarehe za uzalishwaji ndani ya Zanzibar.
Mapema Kaimu Mkurugenzi huyo aliishauri jamii kutumia vyakula vilivyothibitishwa na kutoa mashirikiano pale wanapokuwa na mashaka juu ya bidhaa zilizopo sokoni kwani usalama wa chakula ni jukumu la kila mtu.
Katika ukaguzi uliofanya na wakala wa chakula, dawa na vipodozi wamefanikiwa kuyatoa sokoni zaidi ya makopo elfu moja ya bidhaa hiyo yakiwa na maandishi yanayosomeka “NOT FOR RESALE IN TANZANIA”, yaani yasiuzwe tena nchiniMAELEZO YA PICHA