Msaidizi wa Mkuu wa Usalama Barabarani Wilaya ya Mbozi Mkaguzi wa Polisi Kisbert Kapondo amewataka Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Vwawa Day kuzingatia sheria za usalama barabarani pindi waendapo na watokapo shule ili kujiepusha na ajali za barabarani.
Kauli hiyo imetolewa Mei 10, 2024 wakati akitoa elimu ya umuhimu wa kufuata sheria za usalama barabarani.
“Mkiwa mnakuja na kutoka shule mnapaswa kupita kwenye vivuko vya watembea kwa miguu pia matakiwa kuwa makini kwa kuangalia pande zote mbili za barabara zaidi ya mara moja na ukiwa unavuka usikimbie unatakiwa utembee ili ujiepushe na kujikwaa ambapo kunaweza kukusababishia madhara na kukatisha ndoto za masomo na maisha yako ya baadae” alisema Mkaguzi Kapondo.
Nae, Kiongozi wa umoja wa wanafunzi shuleni hapo Sheila Issa amelishukuru Jeshi la Polisi kwa kuendelea kuwajengea uelewa wa mambo mbalimbali ikiwemo sheria za usalama barabarani ili kuepukana na ajali zinazoweza kuepukika.