Na WAF – Dodoma
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amepiga marufuku kwa watendaji wa Wizara ya Afya na wadau wake kutowauzia
Wajawazito vitabu vya kliniki huku akimuagiza Katibu Mkuu kuhakikisha vitabu vinapatikana muda wote.
Waziri Ummy amesema hayo Mei 10, 2024 jijini Dodoma katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma wakati hafla ya kuzindua zoezi la usambazaji wa kadi za maendeleo ya Kliniki kwa wajawazito na watoto.
“Nimarufuku kuuza vitabu hivi kama ilivyo andikwa kwenye kitabu hiki, Rais Samia ametupatia fedha kwa ajili yakuchapisha vitabu hivi hivyo asipatikane mtu atayepata uchu wa kuuza tena.” Amekemea vikali Mhe. Ummy
Aidha, Waziri Ummy amesema suala la mama na mtoto ni kipaumbele cha Serikali kwa sasa ili kuweza kufikia malengo ya milenia, hivyo ugawaji wa kadi za mama mjamzito, watoto wa kike na wakiume ni moja ya hatua zakufikia malengo hayo.
Kuhusu vitabu vilivyo tengenezwa, Waziri Ummy amesema wamezingatia mahitaji yaliopo ambapo inakadiriwa kwa mwaka kuwa na wajawazito Milioni 2 na watoto wanao zaliwa ni Milioni 2.
“Kwa sasa mbali yakuboresha Kadi zetu na kuzitofautisha baina ya ile ya mama mjamzito, mtoto wa kiume itakayo kuwa na rangi ya Bluu na ya mtoto wa kike itakayokuwa na rangi ya Pinki.” Amesema Waziri Ummy
Katika hatua nyingine, Waziri Ummy amewataka wa-mama wajawazito kuwahi Kliniki mapema katika miezi Mitatu ya Kwanza ili kuweza kumsadia Mama kujua maendeleo ya ukuaji wa mtoto awapo tumboni.
Awali akimkaribisha Waziri Kuzungumza, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe, alisema kama kuna kero ilikuwa ikimkwaza Waziri ni pamoja na kukosekana kwa kadi za kliniki hivyo uchapishaji huo ni sehemu yakwenda kuondoa kero hiyo.
“Wakinamama wamekuwa wakiacha kwenda Kliniki kwakuwa walikuwa wanauziwa kadi hizi, sasa Serikali imechapisha kadi zakutosha na tutaendelea kufanya hivyo kila mwaka ili kumuepusha Mama na kadhia hii.” Amesema Dkt. Magembe
Awali akitoa salam za Mkoa na kwa niaba ya Mikoa Mingine, Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma amesema, Mkoa huo umekuwa mstari wa mbele kupunguza vifo vya mama na mtoto hivyo ujio wa kadi hizo mpya utakuwa kichocheo cha uimarishaji wa huduma katika mkoa wao.
Kwa sasa Serikali imesha chapisha jumla ya vitabu Milioni 1.2 vikiwepo vya wamama wajawazito laki 600,000 na watoto wa kiume laki 300,000 samba na watoto wa kike laki 300,000 ikiwa ni makadirio ya nusu Mwaka.