Naibu Makamu Mkuu Taaluma Chuo cha Mkatifu Augustino (SAUT) Kampasi ya Mwanza Hosea Rwegoshora akifungua mafunzo ya siku tatu ya kuwajengea uwezo washauri wa wanafunzi Jijini Mwanza.
Picha ya pamoja
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Washauri wa wanafunzi wamehimizwa kuendelea kuwasaidia wanafunzi katika masuala ya maadili pindi wawapo vyuoni hatua itakayosaidia kutimiza ndoto zao za kielimu.
Rai hiyo imetolewa jana Mei 8, 2024 na Naibu Makamu Mkuu Taaluma Chuo cha Mkatifu Augustino (SAUT) Kampasi ya Mwanza Profesa Hosea Rwegoshora, wakati wa kufungua mafunzo ya washauri wa wanafunzi yaliyoandaliwa na Chama cha Ushauri na Uelekezi kwa Washauri wa Wanafunzi vyuo vya elimu ya juu Tanzania (TACOGA 1984).
Mafunzo hayo ya siku tatu yanafanyika katika Hoteli ya Adden Palace iliyoko Wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza
Profesa Rwegoshora amesema vyuo vinapokea wanafunzi wengi wanaotoka kwenye familia mbalimbali hivyo ni vyema washauri wajikite kwenye suala la elimu ya maadili ikiwemo kuwaasa kuachana na tamaa ya mali.
“Familia zinatofautiana kipato wanafunzi wanapokuwa vyuoni wanakuwa na tamaa za vitu mbalimbali hivyo jitahidini kuwashauri ili waweze kuepukana na vishawishi hivyo”, amesema Rwegoshora
Amesema baadhi ya wanafunzi wanaingia vyuoni wakiwa wadogo hivyo wanashindwa kujisimamia kwenye mazingira hulia ambayo yanaweza kumpotezea dira ya masomo.
Kwaupande wake Mwenyekiti wa TACOGA 1984 Sophia Nchimbi, amewaasa wanafunzi kuzingatia masomo ili waweze kujiepusha na changamoto za ushoga,madawa ya kulevya, mahusiano pamoja na utoro wa kuhudhuria vipindi.
“Masuala ya teknolojia yamekuwa ni mapana sana kunamambo mengi yanayopelekea wanafunzi kuacha masomo hivyo tunawashauri wanapokwama wawaone washauri walioko kwenye vyuo ili waweze kuwasaidia”, amesema Nchimbi
Rhoda Aroko ni Mkurugenzi wa huduma za wanafunzi Chuo Kikuu Dodoma, amesema mafunzo hayo yanampa wigo mpana wa kujifunza vitu mbalimbali vinavyowahusu wanafunzi katika kusoma kwao na makuzi yao wanapokuwa chuoni.