Mratibu elimu katika kata ya Mlingotimashariki wilayani Tunduru Elice Banda katikati,akimsikiliza Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Tunduru Mchanganyiko Sabila Lipukila kushoto,kuhusu ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya elimu katika shule hiyo yenye watoto zaidi ya 1,738 kati yao wanafunzi 43 ni wenye mahitaji maalum,kulia Mwalimu wa shule hiyo Ambilikile Mwandembo.
Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Tunduru Mchanganyiko wilayani Tunduru Sabina Lipukila akiongea na baadhi ya wanafunzi wa darasa la saba wa shule hiyo juu ya umuhimu wa kutunza miundombinu ya elimu inayojengwa katika shule hiyo baada ya serikali kutoa zaidi ya Sh.milioni 300.
Nyumba ya kuishi familia mbili za walimu wa shule ya msingi Tunduru Mchanganyiko iliyojengwa kwa fedha kutoka serikali kuu ambayo itawawezesha walimu kuishi karibu na eneo lao la kazi.
Na Muhidin Amri,
Tunduru
WANAFUNZI wa shule ya msingi Tunduru Mchanganyiko wilayani Tunduru,wameishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, kuwajengea bweni la kuishi na nyumba moja ya walimu.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake,Samia Shabani wa darasa la saba alisema,bweni hilo ni muhimu hasa kwa wenzao wenye ulemavu kwani watapata muda mwingi wa kujisomea kwa kuwa wataishi hapo shuleni,tofauti na sasa ambapo wanatoka majumbani kwao.
Aidha,ameiomba serikali kupitia wizara ya elimu na wadau mbalimbali kujitokeza kujenga na kuboresha miundombinu mingi zaidi katika shule hiyo kwani mahitaji yao ni makubwa kutokana na wingi wa wanafunzi waliopo.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Sabina Lupukila amesema,serikali imetoa kiasi cha Sh.milioni 302 kati ya fedha hizo Sh.milioni 246 zimetoka serikali kuu na Sh.milioni 56 zimetolewa na Halmashauri ya wilaya Tunduru.
Lipukila alisema,Sh.milioni 80 zimetumika kujenga bweni,Sh.milioni 50 kujenga nyumba moja ya walimu ya familia mbili,Sh.milioni 60 kujenga uzio na Sh.milioni 56 kwa ajili ya matundu 32 ya vyoo.
Aidha alieleza kuwa,Sh.milioni 56 zilizotolewa na Halmashauri ya wilaya Tunduru, Sh.milioni 41 zimetumika kumaliza ujenzi wa miradi hiyo iliyoanzishwa na serikali kuu na Sh.milioni 15 kwa ajili ya kununua vifaa kama vile magadoro na vitanda
Alisema,bweni lina uwezo wa kuchukua watoto 80 na katika awamu ya kwanza litatumika kulala watoto wa kike wakati serikali ikiendelea na mchakato wa kujenga bweni lingine la watoto wa kiume.
Alisema, kwa sasa shule ya Tunduru Mchanganyiko ina wanafunzi 1,738 kati yao wanafunzi 43 ni wa elimu maalum kuanzia darasa la awali hadi la saba ambao wanatoka nyumbani na kwenda shule kila siku.
Lipukila alisema,ujenzi wa bweni hilo ni mpango wa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan wa kuwajali watoto wenye mahitaji maalum na kuboresha mazingira ya elimu ili kuhamasisha watoto kupenda kusoma na wazazi kupeleka watoto wao shule kwa ajili kupata haki yao ya msingi.
Alisema,serikali inatambua umuhimu wa kuwa na mazingira mazuri ya kusoma ili kuwawezesha watoto wenye mahitaji maalum kusoma bila vikwazo vyovyote kutokana na changamoto zao za kimaumbile.
Alisema, bweni hilo ni dawa itakayotibu watoto wote wenye mahitaji maalum waliopo katika wilaya ya Tunduru kutopenda kusoma na wengine kuacha shule kwani sasa kuna sehemu nzuri na rafiki itakayowawezesha kutimiza ndoto zao.
“watoto wenye ulemavu sio kwamba hawana ndoto,lakini changamoto kubwa imetokana na mazingira magumu kwa baadhi ya wazazi,natoa wito kwa wazazi na walezi wote wenye watoto wenye mahitaji maalum wawalete watoto wao kwenye shule hii”alisema.
Mratibu elimu kata ya Mlingoti Mashariki Erith Banda,ameishukuru serikali kujenga bweni la wanafunzi wenye mahitaji maalum na nyumba moja ya kuishi walimu.
Alisema,bweni hilo litamaliza adha kwa watoto wanaoishi mbali na shule kutumia muda mrefu kila siku kwenda kufuata masomo na kuepukana na changamoto mbalimbali za njiani.
Ambilikile Mwandembo anayefundisha watoto wenye ulamavu alisema,watoto hao wamegawanyika kwenye makundi matatu ambayo ni walemavu wa akili,ulemavu wa kusikia,mabubu,wenye uono hafifu na walemavu wa ngozi.
Alisema,watoto walemavu wanafundishika hivyo wazazi wachae tabia na kasumba ya kuwaficha watoto hao nyumbani,badala yake wawapeleke shule wakapate haki yao ya msingi.