Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula MNEC amesaidia ujenzi na ukarabati wa muda wa miundombinu ya barabara ya Msumbiji-Nyasaka kwa kumwaga vifusi na kuvisambaza vitakavyosaidia barabara hiyo kupitika kwa urahisi na wepesi
Akizungumza wakati wa zoezi la ukarabati wa barabara hiyo, Katibu wa Mbunge Ndugu Charles David Karoli amesema kuwa Mbunge anatambua changamoto za ubovu wa barabara katika maeneo mbalimbali ya Jimbo kufuatia mvua zinazoendelea kunyeesha na kwamba Rais Mhe Dkt Samia Suluhu Hasan amekwishatoa fedha kwaajili ya urejeshaji wa miundombinu iliyoharika na mvua pamoja na jitihada za taasisi za wakala wa barabara za mjini na vijijini TARURA akaona ipo haja ya kutumia fedha za mfuko wa Jimbo kutafuta suluhu ya muda mfupi ili barabara hiyo iweze kupitika vizuri
‘.. Mbunge wetu anatambua adha tunazokutana nazo za miundombinu ya barabara iliyoharika kutokana na mvua na kila siku anapopata nafasi bungeni amekuwa akiyasemea, Pamoja na hivyo akaona ipo haja ya kutafuta njia ya muda mfupi ya kuzifanya barabara zetu zipitike wakati tukisubiria matengenezo ya kudumu ..’ Alisema
Aidha Ndugu Karoli amewataka wananchi wa Jimbo hilo kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kumshukuru Rais Mhe Dkt Samia Suluhu Hasan kwa fedha za maendeleo
Nae Mwenyekiti wa CCM kata ya Kawekamo Ndugu Saadi Lwekaka mbali na kumpongeza Mbunge Dkt Angeline Mabula kwa namna anavyotatua kero za wananchi wake, ameongeza kuwa barabara hiyo ilikuwa kero Kwa muda mrefu kiasi cha kukwamisha shughuli za kiuchumi za wananchi wa eneo hilo na changamoto kwa mama wajawazito wakati wa kujifungua
Raphael Mganga Mlumba ni kati ya wananchi wanaoishi eneo la msumbiji kata ya Kawekamo ambapo amemshukuru Dkt Angeline Mabula kwa kuguswa na kuamua kutatua kero ya ubovu wa barabara iliyokuwa ikiwakabili huku akitaka viongozi wengine wa mitaa na kata kuiga mfano huo na kutekeleza wajibu wao badala ya kusubiria kila changamoto itatuliwe na mbunge