Mwenyekiti wa Kamati ya Kimkakati ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Brigedia Jenerali Hassan Mabena,akikagua mradi wa kilimo cha mchikichi katika Kikosi cha 821 KJ Bulombora mkoani Kigoma mara baada ya kufanya ziara yake ya kukagua mradi huo.
Na.Alex Sonna-KIGOMA
JESHI la Kujenga Taifa (JKT) katika Kikosi cha 821 Bulombora wamezalisha miche takribani 300,000 na kuigawa bure kwa wakulima wakubwa, wa kati na mtu mmoja mmoja na kupitia vyama vya ushirika kwa halmashauri zote za Mkoa wa Kigoma.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kimkakati ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Brigedia Jenerali Hassan Mabena,wakati wa ziara yake ya kukagua mradi wa kilimo cha mchikichi katika Kikosi cha 821 KJ Bulombora mkoani Kigoma.
Amesema baada ya maagizo kutoka Serikalini walishirikiana na taasisi ya tari katika kuandaa vitalu ambavyo viliwasaidia kuandaa miche iliyokwenda kutumika katika kwa wakulima mbalimbali.
“Zoezi hili limekwenda vyema na miche zaidi ya 300,000 imegawiwa kwa wakulima bure na maofisa ugani katika kata walisimamia kuhakikisha kuwa inapandwa kitaalamu kwenye mashamba ya wakulima,”amesema Brigedia Jenerali Mabena
Brigedia Jenerali Mabena ambaye Mkuu wa Tawi la Utawala la JKT, amesema wamejiwekea malengo ya kuhakikisha kuwa wanafikia ekari 2000 hadi kufikia mwaka 2024/25 na kwamba hadi sasa wameandaa na kupanda ekari 1100.
“Wenzetu wa TARI (Taasisi ya Utafiti wa Kilimo) Mkoa wa Kigoma wapo hapa kuhakikisha kuwa wanashirikiana na kikosi kuhakikisha kuwa miche hii inakua na kama kuna changamoto zozote zile basi tuweze kuchukua hatua ili kufikia malengo tuliojipangia,”amesema.
Akizungumza kuhusu unufaika wa vijana wakujitolea na wale wa kwa mujibu wa sheria , Brigedia Jenerali Mabena amesema vijana wanaolelewa na JKT, mbali ya kufundishwa mafunzo ya uzalendo, ukakamavu wanafundishwa shughuli za kilimo, stadi za maisha pamoja na ujasiriamali.
Amesema katika mafunzo ya kilimo, vijana hao wamehusika katika hatua zote za kilimo cha chikichi ikiwemo kuandaa miche hadi kupanda.
Akielezea kuongeza thamani kwa mazao yanayozalishwa, Brigedia Jenerali Mabena amesema kupitia shamba darasa na mashine ndogo zilizopo katika kikosi hicho, vijana hao wameelekezwa namna ya kuchakata mafuta ya kula.
Amesema pia wameongezewa maarifa na kufundishwa jinsi ya kuongeza thamani mbegu pia zinazobakia kwa kutengeneza sabuni ambazo hutumika katika shughuli mbalimbali za usafi.
Aidha, Brigedia Jenerali Mabena amesema mpango wa kuongeza thamani kwa mazao yanayozalishwa kwenye vikosi na baadhi yake vimeshafungua viwanda vidogo vya kuchakata mafuta ya alizeti kwa ajili ya matumizi ya vikosi na majirani wanaowazunguka.
“Lakini pia mashudu kwa maana ya mabaki yanayotokana na alizeti yamekuwa yakichanganywa na virutubisho vingine kwa ajili ya kupata chakula cha mifugo. Sote tunafahamu mbali na kilimo Jeshi la Kujenga Taifa linajishughulisha na ufugaji wa ng’ombe, mbuzi, kondoo, kuku,”amesema.
Amesema tathimini imeshafanyika na maeneo yameshafanyiwa tathimini ( survey) kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vikubwa vya kuongeza thamani na kuwa wakipata fedha watakwenda kujenga.
Ametoa mfano wa maeneo waliyokwenda kuyatazama kuwa ni Kikosi cha JKT Chita,mkoani Morogoro ambapo wanalima mpunga kwa kutumia teknolojia ya kisasa na kuwa wakiweza kulima ekari zote 12,000, watahitaji kuwa na viwanda.
“Eneo lile limeshatengwa pale na tiyari hata ule mchakato wa kufuatilia katika baadhi ya nchi kuona kuwa kiwanda amcaho wakiweza umeshafanyika na pia hata katika vikosi ambavyo vinalima mazao mbalimbali kuweza kuongeza thamani. Kwa mfano hapa kwenye mchikichi kuweza kuwa na kiwanda kikubwa kitakacvhoweza kuchakata mafuta na mabaki kwenda kutumika kuzalisha,”amesema.
Kuhusu gharama, amesema zinatofautiana kati ya kiwanda na kiwanda ambapo kiwanda wanachotarajia kukijenga Chita mkoani Morogoro kinatarajiwa kugharimu Sh3 bilioni.
Amesema kiwanda hicho kitakuwa na sehemu ya kutengeneza chakula cha kuku.
Kwa upande wake Kamanda Kikosi cha 821 KJ Bulombora, Luteni Kanali Juma Hongo,amesema wamekuwa wakipokea maombi ya miche ya michikichi kutoka maeneo mbalimbali na hadi kufikia jana walikuwa wamegawa miche zaidi 300,000.
“Kama SUA (Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine), kimechukua miche na wametueleza maendeleo ni mazuri sana lakini kuna mabalozi ambao wako nje ya nchi wametuletea mrejesho mambo ni mazuri, kumekuwa na mahitaji makubwa. Hii inaonyesha kuwa JKT imetekeleza vyema maagizo ya Serikali,”amesema.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kimkakati ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Brigedia Jenerali Hassan Mabena,akizungumza wakati wa ziara yake ya kukagua mradi wa kilimo cha mchikichi katika Kikosi cha 821 KJ Bulombora mkoani Kigoma.
Kamanda Kikosi cha 821 KJ Bulombora, Luteni Kanali Juma Hongo,akielezea jinsi walivyojipanga kuzalisha miche ya michikichi kwa ajili ya kuwagawia wananchi miche hiyo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kimkakati ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Brigedia Jenerali Hassan Mabena,akikagua mradi wa kilimo cha mchikichi katika Kikosi cha 821 KJ Bulombora mkoani Kigoma mara baada ya kufanya ziara yake ya kukagua mradi huo.
Muonekano wa mbegu za kisasa za mchikichi zinazozalishwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) katika Kikosi cha 821 Bulombora mkoani Kigoma.