NA VICTOR MASANGU,KIBAHA
Kaya zipatazo 164 zilizopo katika eneo la Ruvu station lililopo Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani wameondokana na changamoto ya maji baada ya kukamilika kwa mradi wa kisima cha maji chenye uwezo wa kutoa lita 11,820.
Akitoa taarifa kwa kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru kitaifa Meneja wa Mamlaka ya maji safi na usafi wa Mazingira vijijini (RUWASA) Debora Kanyika alisema kwamba kisima hicho kitakuwa na urefu wa mita 43.
Meneja Kanyika alibainisha kwamba mradi huo ambao utekelezaji wake ulianza tangu mwaka 2023 una uwezo wa kuhifadhi maji lita zipatazo elfu 50,000 juu ya mnara wa mita 12.
Kadhalika Meneja huyo alibainisha kuwa mradi huo wa kisima utakuwa na na vituo vipatavyo saba ambavyo ni kwa ajili ya kuweza kuchotea maji.
“Mradi huu una urefu wa mita zipatazo mita 43 na kwamba mnara wa mita 12 pamoja na vituo vipatavyo saba vya kuchotea maji kwa wananchi sambamba na mitambo ikiwa na mitambo ya kutandaza mabomba yenye kipenyo cha kuanzia inchi tatu hadi robo tatu,”alisema Meneja huyo.
Kadhalika alisema kwamba mradi huo umegharimu kiasi cha shilingi milion 328 kupitia mfuko wa Taifa wa maji wa (NWF).
Aidha Meneja huyo aliongeza kuwa utekelezaji wa mradi umeongeza hali ya upatikanaji wa maji kwa asilimia moja kwa Wilaya ya Kibaha na sasa huduma hiyo imefikia asilimia 78.
Pia alifafanua kwamba mradi huo ni moja ya utekelezaji wa kampeni ya Rais wa awamu ya sita Dkt.Samia Suluhu Hassan ya kumtua ndoo mama kichwani.
Katika hatua nyingine Meneja alibainisha kwamba mradi huo umeweza kutoa fursa ya ajira kwa wananchi wapatao 63 ambao wanatoka katika maeneo mbali mbali ya Wilaya Kibaha.
Kwa upande wake Kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru Kitaifa Godfrey Mzava ameridhishwa na meadi huo wa maji na kuwapongeza kwa dhati uongozi wa Ruwasa kwa kazi ambayo wanaifanya katika kuwahudumia wananchi.
Kadhalika aliwahimiiza viongozi wa Ruwasa kuhakikisha kwamba wanayafanyia marekebisho baadhi ya mambo katika mradi huo ikiwemo upatikanaji wa Jenereta.