Wananchi wa mkoa wa Arusha wakiendelea kupata huduma katika banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa kambi maalumu ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services iliyokuwa ikifanyika katika maonesho ya Kimataifa ya usalama na afya mahali pa kazi na kumalizika jana jijini Arusha. Jumla ya watu 672 wamepatiwa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo.
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Odilia Njau akimpa elimu kuhusu shinikizo la damu mwananchi aliyetembelea banda la taasisi hiyo wakati wa kambi maalumu ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services iliyokuwa ikifanyika katika maonesho ya Kimataifa ya usalama na afya mahali pa kazi na kumalizika jana jijini Arusha. Jumla ya watu 672 wamepatiwa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo.
Picha na: JKCI
Na: Mwandishi Maalumu – Arusha
Watu 77 wamepewa rufaa kufika katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwaajili ya kufanyiwa vipimo vikubwa vya kuchunguza moyo na wengine kufanyiwa upasuaji wa moyo.
Rufaa hizo zimetolewa wakati wa kambi maalumu ya siku 8 ijulikanayo kama Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services iliyokuwa ikifanyika katika maonesho ya kimataifa ya usalama na afya mahali pa kazi na kumalizika jana katika viwanja vya General tyre vilivyopo jijini Arusha.
Akizungumza na waandishi wa habari daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dickson Minja alisema watu wengi waliowahudumia na kuwakuta na matatizo ya shinikizo la damu, sukari na magonjwa ya moyo walikuwa hawajijui na hawakuwa wakitumia dawa.
“Kupitia vipimo tulivyovifanya wakati wa maonesho haya, watu 147 tumewakutwa na shinikizo la damu ambapo kati yao watu 85 hawakuwa wanajua kama wana matatizo ya shinikizo la damu hivyo hawakuwa wanatumia dawa”,
“Watu 23 tuliwakuta na magonjwa ya moyo ambayo ni matatizo ya valvu za moyo (Rheumatic heart disease), changamoto za mfumo wa upelekaji wa damu kwenye moyo (Ischemic heart disease), moyo kutanuka, na shinikizo la juu la damu”, alisema Dkt. Dickson
Dkt. Dickson alisema katika maonesho hayo wameweza kuwafanyia vipimo vya magonjwa ya moyo, shinikizo la damu na sukari kwenye damu wananchi 672 ambapo kati yao watu 170 sawa na asilimia 25 wamekutwa na magonjwa mbalimbali ya moyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi wa Arusha wameishukuru taasisi ya JKCI kwa kuwafikishia huduma karibu, kuwapa nafasi ya kupima afya na kupata elimu ya kujikinga na magonjwa ya moyo.
John Eliud alisema haikuwa rahisi kwake kuchukua uamuzi wa kupima moyo kutokana na mtindo wa maisha yake kwani amekuwa akitumia vilevi mbalimbali ambavyo mara nyingi amekuwa akiambiwa si salama kwa afya.
“Nawashukuru sana JKCI nimepima sukari, presha na moyo na vyote nimekuta viko sawa, daktari kanishauri kupunguza na baadaye kuacha kabisa kutumia vilevi ninavyotumia ili kuulinda moyo wangu”, alisema John
Naye Denis Nyakutanwa aliipongeza Taasisi ya JKCI kwa kazi kubwa inayofanya ya kutoa huduma za uchunguzi wa afya kwa jamii na kuiomba kuendelea kuwafikia wananchi kwani wengi wao hawana uwezo wa kuifikia kwaajili ya kufanya uchunguzi wa afya.
“Nawapongeza sana kwa kutufikia, lakini nimesikia gharama za matibabu ya moyo ni kubwa. Naiomba Serikali iangalie namna ya kuwezesha upatikanaji wa vifaa vya matibabu ya moyo kirahisi ili kupunguza gharama za matibabu ya moyo”, alisema Denis.