Afisa Usafirishaji  Idara ya udhibiti huduma za  usafiri Majini Celina  Mokiti  akizungumza na waandishi wa habari mkoani Arusha .
Afisa Uhusiano Mwandamizi  wa Shirika la Uwakala Tanzania (TASAC) Amina Miruko akizungumza  na waandishi wa habari kuhusiana na shughuli zinazofanywa na shirika hilo. 
……..
Happy Lazaro,Arusha.
Arusha .Watumiaji wa Usafiri wa Majini nchini  wametakiwa kujisajili katika Shirika la uwakala  wa Meli Tanzania(TASAC) kutokana  na wengi kutokufahamu haki zao hivyo kushindwa kupata msaada pale wanapopatwa na matatizo.
Rai hiyo imetolewa na Afisa Usafirishaji  Idara ya udhibiti huduma za  usafiri Majini Celina  Mokiti    wakati akieleza baadhi ya changamoto wanazokutana nazo katika Shirika hilo katika maonyesho ya Usalama na Afya mahali Pakazi yaliyoandaliwa na  Wakala wa Usalama na Afya mahali Pakazi nchini (OSHA) yanayoendelea Mkoani Arusha.
Hata hivyo  amesema kuwa, ni muhimu mteja kufahamu haki zake kwa lengo la kuondoa migogoro kati ya watoa huduma na wateja. 

Amesema  huduma zinazotolewa na wakala huyo wa Meli nchini (TASAC) ni pamoja na kudhibiti watoa huduma, kudhibiti mawakala wa meli, kudhibiti mawakala wa ugomboaji na uondoshaji mizigo baharini, kudhibiti wakusanyaji na watawanyaji mizigo.

Huduma zingine ni kudhibiti watoa huduma ndogondogo bandarini, kudhibiti wahakiki bandarini, sambamba na kudhibiti wanaotoa leseni, kuhuisha na kufuta leseni, kuweka viwango vya huduma na vigezo kwa watoa huduma.

Kwa upande wake Afisa Uhusiano Mwandamizi Shirika la Uwakala Tanzania (TASAC) Amina Miruko, ameeleza kuwa wanafanya kazi zao kwa mujibu wa sheria ili kuhakikisha usalama wa abiria, vyombo na mizigo kwa viwango vya kimataifa.

Aidha Miruko  amesema kuwa,wana Jukumu la kuhakikisha Usalama wa vyombo vya Usafiri wa Majini lakini pia Jukumu lingine ni kuratibu utafutaji na uokoaji pale inapotokea dharura yoyote.

Ameongeza kwamba licha ya usimamizi huo, wanahakikisha kuwepo kwa vifaa vya uokoaji ili kuepuka ajali zisizo za lazima na kuwa na vyombo vya ukaguzi kwa lengo la kubaini uharifu.

Amefafanua kuwa, (TASAC) ina majukumu ya kuratibu utafutaji na  uokoaji inapotokea dharura,  TPA na wadau mbali mbali wa uokoaji huwa wanahusishwa ikiwa ni pamoja na Mamlaka ya Usafiri wa Maji Zanzibar (ZMA) ili kuokoa abiria na mali zao.

Aidha ameongeza  kuwa ,TASAC kwa kushirikiana na wadau wengine wameungana pamoja katika kutoa mafunzo mbalimbali yahusuyo Usalama na Afya mahali pakazi huku Mratibu mkubwa wa Maonesho hayo akiwa ni OSHA.

Maonesho ya Usalama na Afya mahali Pakazi yalianza Mapema wiki iliyopita mkoani Arusha Katika Viwanja vya General Tyre vilivyopo njiro mkoani Arusha  ambapo Kilele chake kilikuwa April 28 mwaka huu  huku shughuli za maonesho zikitarajiwa Kuhitimishwa rasmi leo  April 30.