MKURUGENZI Mkuu Tume ya Umwagiliaji Bw. Raymond Mndolwa, amesema katika kipindi cha mwaka 2022/2023 na mwaka 2023/2024, Serikali iliidhinisha sh. bilioni 361.5 mfululizo za kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi na ukarabati pamoja na upembuzi yakinifu wa miundombinu ya umwagiliaji.
Mkurugenzi huyo amyebainisha hayo leo Aprili 30,2024 Jijini Dodoma wakati akizungumza na washiriki wa hafla ya utiaji saini mikataba 20 ya miradi ya umwagiliaji yenye thamani ya sh. bilioni 258.11 ambayo itatekelezwa kwa kutumia washauri elekezi na wakandarasi wa ndani na wa nje.
“Katika mwaka 2022/2023, Tume ilipanga kutekeleza miradi 135 ambapo 69 kati ya hiyo ni ya ujenzi na ukarabati na 66 ni ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Katika mwaka 2023/2024, Tume ilipanga kujenga, kukarabati na kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina katika miradi 647,” amesema.
Aidha amemuhakiki Waziri Mkuu kuwa tume hiyo haina changamoto yoyote bali kazi yao kubwa ni kuzishughulikia na kumuomba waendelee kupelekewa hela kwaajili ya kuwasha injini ya pili kwani ya kwanza tiyari wamekwisha kuiwasha.
Amesema katika miradi 20 iliyosainiwa 14 ni ya ujenzi huku kandarasi 2 zikiwa ni za wakandarasi wa nje na iliyosalia ikiwa ni ya wazawa ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Hafla hiyo pia imeshuhudiwa na Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wabunge, wakuu wa Taasisi zailizo chini ya Wizara ya Kilimo na watumishi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji.