Maafisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Odilia Njau na Benson Bisare wakiwapima wananchi shinikizo la damu walipotembelea banda la Taasisi hiyo lililopo katika maonesho ya kimataifa ya usalama mahala pa kazi yanayofanyika katika viwanja vya General tire vilivyopo jijini Arusha.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dickson Minja akimwelezea huduma zinazotolewa katika banda la Taasisi hiyo mwananchi aliyetembelea banda la JKCI wakati wa maonesho ya kimataifa ya usalama mahala pa kazi yanayofanyika katika viwanja vya General tire vilivyopo jijini Arusha.
Picha na: JKCI
Na: Mwandishi Maalumu – Arusha
Wananchi wa Mkoa wa Arusha wajitokeza kufanya uchunguzi wa magonjwa ya moyo, shinikizo la damu, sukari kwenye damu na uwiano wa urefu na uzito katika banda la Tasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Uchunguzi huo unafanyika katika banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) lililopo katika maonesho ya kimataifa ya usalama na afya mahali pa kazi katika viwanja vya General tire vilivyopo jijini Arusha.
Akizungumza alipotembelea banda la JKCI mkazi wa Arusha Aika Msuya alisema amevutiwa kupima moyo wake kwani amekuwa akipata maumivu makali ya kifua tatizo ambalo hajawahi kufuatilia kama ni shida ya moyo au ni tatizo lingine.
“Nashukuru baada ya kufanyiwa vipimo nimekutwa salama na kupewa ushauri wa kuwa nafanya uchunguzi wa afya mara kwa mara, kufanya mazoezi na kula mlo kamili”, alisema Aika
Aika alisema matembezi yake katika maonesho hayo yamekuwa yamafanikio kwani hakutegemea kama angepata nafasi ya kupima moyo kama isingekuwa kupitia maonesho hayo.
Grace Kitundu mkazi wa Arusha alisema yeye kama mama lishe analo jukumu la kuiokoa jamii isipate magonjwa ya moyo kwa kujitahidi kutumia mafuta kidogo ambayo ni safi na salama kwa afya.
“Nimefurahi leo nimefika katika banda la JKCI na kupata elimu nzuri ambayo inaenda kunibadilisha katika kazi zangu kwani sisi kama mama lishe tumekuwa tukiandaa vyakula vya wateja wetu bila ya kuangalia usalama wa afya”, alisema Grace
Grace alisema anaenda kuwa mwalimu kwa wenzake wanaofanya biashara ya chakula hasa eneo la matumizi ya chumvi nyingi wakati wa kuandaa chakula ili kuwalinda wateja wanaowahudumia.
Naye Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dickson Minja alisema Taasisi hiyo itakuwepo katika maonesho hayo hadi tarehe 30 Aprili 2024 ikitoa huduma za uchunguzi wa magonjwa ya moyo, shinikizo la damu na sukari kwenye damu kwa watu wote watakaotembelea banda la JKCI bila gharama.
Dkt. Dickson alitoa wito kwa vijana ambao umri wao umeanza kusogea na watu ambao bado hawajapata changamoto za moyo kuchunguza afya zao, kubadili mifumo ya maisha kujikinga kupata changamoto za magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo.