Na Mwamvua Mwinyi, Chalinze
Naibu Waziri wa Utumishi na Utawala Bora ambae pia ni Mbunge wa Jimbo la Chalinze ,Ridhiwani Kikwete amewataka wanafunzi na vijana kuacha matumizi mabaya ya mitandao, mambo yaliyo nje ya tamaduni za kitanzania na badala Yake watumie mitandao hiyo kujifunza na kujipa uelewa zaidi katika masuala ya masomo na elimu.
Aidha amewaasa kusoma kwa bidii kwani elimu ndio nguzo ya maisha yao.
Ridhiwani alitoa rai hiyo alipokuwa akihutubia wahutimu wa kidato cha sita shule ya sekondari ya Lugoba , Halmashauri ya Chalinze, mkoani Pwani.
Aliwaasa wahitimu hao kuhakikisha wanafaulu ili waache deni la kufuatwa na wadogo zao wanaowafuata kwa upande mmoja, wawape heshima walimu na wazazi kwa kufaulu vizuri.
Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo ,Abdallah Sakasa aliishukuru serikali kwa kuendelea kupeleka pesa za elimu bure , vifaa na kuongezeka kwa madarasa na walimu shuleni hapo .
Alimuomba mbunge kuendelea kuikumbuka shule hiyo kwa kuisaidia vifaa na kuongeza mabweni ya wanafunzi.