Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema Serikali imetunga Sheria Maalum No. 18 ya mwaka 2004, mahsusi kwa ajili ya waasisi hao wa Muungano.
Amesema hayo wakati akijibu swali la Mbunge kutoka Baraza la Wawakilishi Mhe. Suleiman Haroub Suleiman aliyetaka kujua mpango ya Serikali katika kuwaenzi na kuwatunza waasisi wa Muungano.
Dkt. Jafo amesema kuwa pamoja na sheria hiyo imetungwa Kanuni ya Mwaka 2005 iliyoweka utaratibu wa namna ya kuwaenzi waasisi wa Muungano ikiwemo kuhifadhi kumbukumbu zao, kazi zao na kueneza falsafa zao.
Amefafanua kuwa Idara Maalumu ya Kuwaenzi Waasisi imeundwa, ikiwa chini ya Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, ikishughulika na usimamizi, ukusanyaji na uhifadhi wa Kumbukumbu na vitu vya waasisi wa Taifa vyenye umuhimu wa kihistoria.
Aidha, Dkt. Jafo ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuhakikisha kuwa kila mwaka kumbukumbu za kifo cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume pamoja na maadhimisho ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zinafanyika.