Wajumbe wa Bodi ya Hospitali wakisikiliza kwa makini maelezo ya mtaalamu katika maabara, kuhusu namna wanavyoendesha shughuli zao.
Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali ya Chuo Kikuu cha Dodoma, Dkt. Saitori Laizer (Mwenye tai, wa pili kulia), akisikiliza kwa makini maelezo ya mtaalamu wa maabara wakati wa ziara ya Bodi hiyo kukagua shughuli zinazofanywa katika Hospitali hiyo. Wengine ni watendaji kutoka vitengo mbalimbali vya Hospitali.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Prof. Lughano Kusiluka (Katikati), akiongoza wajumbe wa Bodi ya Hospitali ya Chuo, kwenye vituo vya matibabu. Kushoto ni Prof. Winester Anderson (Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Mipango, Fedha na Utawala), na kushoto ni Dkt. Boaz Matobogolo (Daktari Mfawidhi wa Hospitali ya Chuo).
Dkt. Boaz(katikati) akitoa maelezo kwa Wajumbe wa Bodi ya Hospitali, walipokuwa wakikagua Jengo jipya la vipimo vya mionzi lililomalizika ujenzi.
Mmoja wa wananchi akifika kupata huduma kwenye moja wapo ya vituo vya huduma katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Dodoma.
……..
Bodi ya Hospitali ya Chuo Kikuu cha Dodoma, imefanya ziara ya kukagua huduma za Hospitali zinazotolewa na Chuo hicho kwa wanafunzi na wananchi wa vijiji jirani vinavyozunguka Chuo hicho.
Bodi hiyo Alhamisi tarehe 18 Aprili 2024, imetembelea Hospitali ya Chuo yenye hadhi ya Wilaya, katika matawi yake matatu: Tawi la Ndaki ya Insia na Sayansi za Jamii ambapo hutolewa huduma kwa wagonjwa wa nje, kwa magonjwa yasiyo ya Upasuaji; Tawi la Ndaki ya Sayansi za Komputa na Elimu Angavu ambalo hutoa huduma za kibingwa za upasuaji na Uzazi, na Kituo kidogo katika Ndaki ya Elimu, ambacho matibabu ya magonjwa madogo madogo.
Akitoa taarifa ya maendeleo ya Hospitali hiyo Mganga Mfawidhi, Dkt. Matobogolo Boaz, amesema, kwa sasa Hospitali hiyo imekuwa ikitoa huduma nyingi za kibingwa kwa wafanyakazi, wanafunzi na wananchi katika maeneo jirani kwa kutumia wataalamu bingwa walioajiriwa na Chuo katika Hospitali hiyo na katika Shule Kuu ya Tiba na Meno, na Shule Kuu ya Uuguzi na Afya ya Jamii. Pia, huduma nyingine zinazotolewa kwenye vituo hivyo ni huduma za vipimo vya maabara.
Aidha, amesema wananchi wengi wamekuwa wakinufaika na huduma za Uzazi na Watoto, ingawa changamoto kubwa ni wananchi wengi wa Dodoma kutofahamu uwepo wa vituo hivyo ili kufika kupata huduma.
“ Wananchi wengi wa Dodoma bado hajatambua uwepo wa Hospitali yetu na baadhi wamekuwa wakidhani uwepo wa Hospitali hii ni kwa wanafunzi tuu na wafanyakazi. Sisi tunahudumia wananchi wote popote wanapotoka” alisisiza
Akizungumzia maendeleo katika ujenzi wa miundombinu, Dkt. Boaz amesema tayari Chuo kimekamilisha ujenzi wa jengo la kisasa la vipimo vya mionzi (Imaging Unit) litakalotumika kutoa huduma na kufundishia; na pindi vifaa vitakapopatikana litaanza kufanya kazi.
Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali hiyo Dkt. Saitori Laizer kwa niaba ya Bodi, amepongeza uwekezaji mkubwa uliofanyika katika Hospitali na hasa kuhakikisha Chuo kinatoa huduma bora na za kisasa. Amesema Bodi imevutiwa na uwekezaji katika ujenzi wa jengo la Vipimo vya Mionzi (Imaging Unit), na kwamba ni kitakuwa kituo cha kwanza cha mfano nchini, na kuitaka Menejimenti ya Chuo kuharakisha upatikanaji wa vifaa ili jengo hilo kuanza kutumika mara moja kwa malengo yaliyokusudiwa.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Lughano Kusiluka, ameihakikishia Bodi hiyo jitihada za Menejimenti za kuendelea kutafuta fedha za kununua na kufunga vifaa, ili jengo hilo lianze kutumika; na kwamba tayari Chuo kiko kwenye hatua za mwisho za kuanzisha kozi ya kuzalisha wataalamu wa vifaa vya Radiolojia ambao sehemu kubwa watakuwa wanufaika wa uwepo wa jengo hilo.