MKUU wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU), Mkoa wa Dodoma,Bw.John Joseph wakati ,akitoa taarifa kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Aprili 18,2024 jijini Dodoma kuhusu taarifa ya miezi mitatu za kazi za Taasisi hiyo.
MKUU wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU), Mkoa wa Dodoma,Bw.John Joseph wakati ,akitoa taarifa kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Aprili 18,2024 jijini Dodoma kuhusu taarifa ya miezi mitatu za kazi za Taasisi hiyo.
Na.Alex Sonna-DODOMA
KATIKA kipindi cha Miezi mitatu kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mkoa wa Dodoma imefuatilia miradi 62 yenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni 51 katika sekta za elimu,ujenzi, afya,Maji na Utawala.
Hayo yamesemwa leo,Aprili 18,2024 jijini Dodoma na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma Bw.John Joseph wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu taarifa ya miezi mitatu za kazi za Taasisi hiyo.
Amesema jumla ya miradi 42 ya elimu imefanyiwa ufuatiliaji, ujenzi miradi 10,Afya Miradi 5,Maji Miradi 3 na utawala Miradi 2.
“Katika ufuatiliaji huu wa miradi ya maendeleo tumebaini kuwepo kwa mapungufu kadhaa katika miradi 10 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 9.9 ,”amesema Bw.Joseph
Mapungufu yaliyobainika ni matumizi ya nondo zilizo chini ya kiwango,matumizi ya mbao hafifu katika milango na ujenzi kutoendana na fedha zilizotumika..
Aidha Bw.Josepha ametaja mapungufu mengine waliyobaini kuwa ni baadhi wa Wazabuni kulipwa fedha kabla ya kuwasilisha vifaa, matofali na mabati kutofanyiwa ukaguzi wakati wa kupokelewa kama kanuni za manunuzi zinavyoelekezwa.
“Kutokana na mapungufu hayo yamesababisha kufunguliwa kwa majalada ya uchunguzi nane na elimu na ushauru umetolewa kwa baadhi ya miradi ili wahusika kufanya marekebisho kwa baadhi ya miradi,”amesema
Hata hivyo ameongeza kuwa TAKUKURU imepokea jumla ya malalamiko 129 kati ya hayo Malalamiko 47 hayakuhusu rushwa hivyo walalamikaji walielimishwa na kushauliwa na taarifa kufungwa.
“Malalamiko 82 yalihusu rushwa ambayo yalipelekea kufunguliwa majadala ya uchunguzi,kati ya majadala hayo,uchunguzi wa majadala 19 umekamilika na majadala 4 mashauri yake yamefunguliwa Mahakamani na jalada moja maamuzi yameshatolewa ambapo Mshitakiwa ametiwa hatiani”amesema
Katika hatua nyingine amesema wamejipanga kuongeza kasi ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuziba mianya ya rushwa na ufujaji unaoweza kujitokeza katika utekelezaji wa miradi hiyo.
“Tumejipanga kuongeza kasi ya uelimishaji umma kwa kutumia njia mbalimbali hasa katika makundi ya vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa.Tutazindua shindano la mdahalo wa uelimishaji rushwa juu ya madhara ya rushwa katika shule za Misingi,Sekondari na Vyuo Vikuu vilivyopo katika Wilaya ya Dodoma.”amesema Bw.Joseph
Aidha amesema wamejipanga kuongeza kasi katika kufanya chambuzi za mifumo hasa katika maeneo yanayolalamikiwa zaidi ya utoaji huduma kwa wananchi na katika miradi ya maendeleo inayogusa wananchi
Bw.Joseph ametoa wito kwa kila mmoja wananchi kushiriki katika mapambano dhidi ya Rushwa kwani mapambano dhidi ya Rushwa ni wajibu wa Kikatiba.