Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MKUU wa wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, Fakii Raphael Lulandala amesema mabosi wake ni watatu tuu CCM, Rais Samia Suluhu Hassan na wananchi wa eneo hilo ambao atawatumikia kwa nguvu zake zote.
Lulandala ameyasema hayo mji mdogo wa Orkesumet wakati wa tafrija ya kumuaga aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo Dkt Suleiman Serera na kumkaribisha yeye.
Amesema hatarajii kuwa na mabosi wengine zaidi ya hao watatu ambao atawatumikia kwa unyenyekevu, umakini, uadilifu na umahiri.
“Rais Samia Suluhu Hassan ndiye anasiimama kwa niaba ya wananchi waliomweka madarakani kupitia CCM hivyo nitasimama kutetea hivyo vitu vitatu,” amesema Lulandala.
Hata hivyo, amewataka wakuu wa idara na taasisi kutowanyanyasa watumishi wa ngazi ya chini kwani wote wanafanya kazi ya kumsaidia Rasi Samia kuhudumia wananchi
“Viongozi wa taasisi na wakuu wa idara msiwanyanyase wafanyakazi wa chini yenu na asiwepo kiongozi anayepandisha mabega na kuwafanya waone kazi wanayofanya ni ngumu,” amesema Lulandala.
Amesema Dk Serera alikuwa na utaratibu wa uongozi wake ila naye atakuja na mtindo wake wa uongozi hivyo hawatafanana zaidi ya kuwa wakuu wa wilaya.
“Mimi nitavaa viatu vyangu hivyo suala la viatu kubana au kupwaya halitakuwepo Simanjiro zaidi ya kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo kupitia sekta ya elimu, afya, maji na mengineyo,” amesema Lulandala.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Suleiman Serera, ambaye alikuwa mkuu wa wilaya hiyo amesema hivi sasa yupo kwenye wizara ya furaha.
“Kule tupo kwenye furaha hatuna msongo wa mawazo wala malalamiko ya basi limegonga mifugo ya wafugaji wanakuja kukulalamikia hakuna,” amesema Dk Serera.
Amewataka watumishi wa eneo hilo wasijione wanyonge kuwa Simanjiro kwani yeye amepanda wizarani na Lulandala alikuwa Katibu mkuu wa UVCCM Taifa.
“Simanjiro inaangaliwa kwa jicho la kipekee hivyo fanyeni kazi kwa bidii na siku moja mtaonekana na kutambulika zaidi ya hapo mlipo,” amesema Dk Serera.
Katibu tawala wa wilaya ya Simanjiro, Warda Abeid Maulid amesema watamkumbuka Dk Serera kwa misimamo yake mikali pindi alipokuwa akiwaongoza.
“Tutakukumbuka kwa mambo mengi ikiwemo kupenda uwajibikaji, ukweli na kutatua migogoro ya jamii ya eneo hili,” amesema Warda.