Baraza la Ushindani (FCT) limeandaa mafunzo kwa wadau wake wakiwemo wafanyabiashara, watoa huduma na walaji ikiwemo jamii kwa lengo la kuwaelimisha kuhusu shughuli za Baraza la Ushindani na umuhimu wake katika Uchumi wa Soko.
Akifungua mafunzo hayo Aprili 9, 2024 jijini Arusha., Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Arusha anayehusika na viwanda, biashara, na uwekezaji, Bw. Frank Mmbando, alipongeza juhudi za FCT katika kuimarisha ushindani wa haki na ulinzi wa watumiaji.
“Elimu hii ni muhimu sana kwa wadau wote katika Soko, itawezesha wadau kutambua haki na wajibu wao, kukuza ushindani wa haki, kuongeza uwajibikaji, na kutatua migogoro ya kiushindani kwa ufanisi.”Alisema Bw. Mmbando. “
Bw. Mmbando alihimiza washiriki wa mafunzo hayo kutumia vyema elimu watakayoipata kutatua changamoto au migogoro ya kibiashara inayoweza kutokea kwa kuwa FCT ni chombo kinachosimamia haki kwa watu wote.
Naye Mkuu wa Idara ya Uchumi FCT, Bw. Kulwa Msogoti, ameongeza kuwa Baraza linahamasisha wadau wote wakiwemo wafanyabiashara, wawekezaji, watoa huduma, na walaji ikiwemo jamii wawasilishe mashauri yao kwa ngazi ya rufaa FCT endapo hawajaridhika na maamuzi yanayotolewa na Tume ya Ushindani na Mamlaka za Udhibiti za EWURA, LATRA, TCAA, TCRA na PURA.
Aidha, Bw. Msogoti amesema kuwa FCT inapokea, kusikiliza, na kutoa maamuzi ya rufaa yanayotokana na maamuzi ya vyombo hivi yanayohusiana na masuala ya ushindani wa kibiashara na udhibiti wa huduma mbalimbali kama vile maji, nishati, mawasiliano, usafiri wa nchi kavu na anga katika Soko.
Kwa upande wa Afisa Sheria Mkuu wa FCT, Bi. Hafsa Said, amesisitiza kuwa FCT inatekeleza Sheria ya Ushindani, 2003 na Kanuni za Baraza la Ushindani za mwaka 2012 na Baraza linaweza kutoa adhabu kwa wale wanaokiuka Sheria hii pamoja na Sheria zilizoanzisha Mamlaka za Udhibiti tajwa hapo juu.
Alisisitiza kuwa FCT ni Mamlaka ya mwisho katika Mfumo mzima wa ushindani wa kibiashara na udhibiti wa Soko ambapo mashauri yote ya rufaa yanasikilizwa.
Akieleza utaratibu wa kushughulikia rufaa FCT, Bi. Said, ameelezea kuwa Mtu anayekata rufaa analazimika kuwasilisha barua ya kuomba mwenendo wa shauri, nyaraka zote zilizosikilizwa mara ya kwanza kutoka Tume ya Ushindani au Mamlaka za Udhibiti husika na sababu za rufaa na kuwasilisha mbele ya Baraza na kesi husikilizwa na kutolewa maamuzi ndani ya kipindi kisichozidi miezi sita au kipindi kifupi kulingana na shauri lenyewe.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Afisa Mdhibiti Ubora wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA), Bw. Dismoso Chimbunde, amesema LATRA imeweka utaratibu wa kupokea na kushughulikia malalamiko kutoka kwa abiria kuhusu huduma za usafirishaji na iwapo hawataridhika na uamuzi wa LATRA, wanaweza kukata rufaa FCT ili kuhakikisha ushindani wa haki.
Naye Mwenyekiti wa Daladala jiji la Arusha, Bw. Maulid Abdallah alisema elimu waliopewa na FCT imewasaidia kielewa kuwa wakipeleka malalamiko yao LATRA wakiona wanashindwa kupata mwafaka au maamuzi yatakayowaridhisha watakata rufaa FCT ili kupata suluhu ya kuendeleza biashara zao.
Kwa upande wake Kaimu Afisa Huduma kwa Wateja na Utawala EWURA CCC, Bi Sharifa Lengima amesema elimu iliyotolewa na FCT ni nzuri ili waweze kusaidia wateja na amewashauri wateja kupata elimu katika huduma wanazotumia kwa kuwa Taasisi zipo kwa ajili ya kuwasaidia.