Na Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo
SHEIKH Mkuu wa Mkoa wa Pwani ,Hamis Mtupa ametoa rai kwa watu wanaodhulumu mali za yatima ili kujinufaisha na kuwaacha watoto hao wakitangatanga ,waache dhuluma hiyo kwani ni sawa na kula moto utakaowachoma kesho kiama.
Aidha ameitaka jamii kuwapa Upendo na haki zao ambazo huwa zimeachwa na wazazi waliofariki kwa ajili yao badala ya kuwadhulumu .
Mtupa alitoa rai hiyo, Wilayani Bagamoyo wakati wa dhifa kwa ajili ya watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu, wajane na wazee iliyoandaliwa na Taasisi ya (SHAKIBA) Islamic Foundation ya Bagamoyo.
Alieleza ,baadhi ya watu wamekuwa wakiwanyanyasa na kudhulumu mali za wazazi wao na kuzitumia huku watoto hao wakiwa hawaruhusiwi kuzitumia.
“Watu wanaokula au kujinufaisha na yatima ni sawa na kula moto sawa na kaa la moto kulitia tumboni hivyo moto huo utawachoma na kila watakalolifanya halitafanikiwa,”alisema Mtupa.
“tu anayekula mali ya yatima anamkanusha Mungu siku ya malipo atalipia dhuluma aliyoifanya kwa yatima hao ambao wanahitaji kusaidiwa”
“Tunapaswa kuwafadhi watoto yatima badala ya kuwatesa ili tupate thawabu wawekeni kwenye sehemu yao kwani ukimtunza kumpa faraja na kumlea utajiwekea mahala pema peponi,”alisema Mtupa.
Kwa upande wake mwenyekiti wa SHAKIBA Alhaj Abdul Sharifu alifafanua ,taasisi hiyo ina lengo la kusaidia watu mbalimbali wenye mahitaji wakiwemo wajane, yatima na wazee.
Sharifu alielezea ,tayari wameanzisha kituo cha kulea yatima wapo 124 huku 24 wkiwa wanawasomesha .
Nae mwenyekiti idara ya wanawake Jamila Suleiman alisema kuwa wanawake wanahitaji kusaidiwa na waume zao na siyo kuwapa mizigo wanawake.
Mratibu wa SHAKIBA Taifa Dk Fakhad Mtonga alielezea ,wamekuwa wakitoa elimu ya kukabili vitendo vya ukatili na ukatili wa jinsia, kujitambua na kukabili vitendo viovu na wanatarajia kuanzisha kituo cha afya ambacho wasiojiweza watatibiwa bure.