Msemaji wa klabu ya mpira wa miguu ya Yanga nchini Tanzania Ndugu Ally Kamwe amemfananisha Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula na winga wa timu yake Pacôme Zouzoua kutokana na juhudi zake na kushirikiana na Rais Dkt Samia Suluhu Hasan katika kutatua kero na changamoto za wananchi wa Jimbo hilo
Kamwe ameyasema hayo wakati wa zoezi la ukarabati mdogo wa barabara ya kutoka Redio Free Afrika RFA kuelekea Ilemela Mahakamani ambapo shughuli ya kuilima vizuri barabara na kusambaza vifusi vilivyotolewa na Mbunge Dkt Angeline Mabula kuifanya barabara hiyo iweze kupitika kwa urahisi imetekelezwa huku akiwaomba wananchi wa jimbo hilo kuendelea kuwaunga mkono Rais Dkt Samia na Mbunge Dkt Mabula kwa kazi nzuri wanazozifanya
‘… Sisi kama klabu ya Yanga hii njia tumekuwa tukiitumia mara nyingi tunapokuja kwenye michezo yetu huku Mwanza, Na ni kweli njia hii imekuwa na changamoto, Kupitia hili mmethibitisha kwa vitendo kwamba CCM ni chama cha mfano shida za nchi yetu, changamoto za nchi yetu tunazitatua sisi wenyewe ..’ Alisema
Aidha Ally Kamwe amemshukuru na kumpongeza Mbunge wa Jimbo hilo kwa kuhakikisha changamoto hiyo anaipatia ufumbuzi huku akisisitiza wananchi kushikamana na viongozi wanaojali shida zao katika uchaguzi mkuu wa 2025 akiwemo Rais Dkt Samia na Mbunge Dkt Angeline
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo hilo Mhe Dkt Angeline Mabula amefafanua kuwa amepokea changamoto ya wananchi wa kata ya Ilemela juu ya ubovu wa barabara hiyo na kwamba kwa kuwa vipindi vya mvua vinaendelea ameamua kutoa vifusi na kuikarabati ili iweze kupitika huku akisubiria vipindi vya mvua viishe ili iweze kujengwa kwa kiwango cha Lami kupitia mipango na bajeti ya wakala wa barabara za mjini na vijijini wilaya ya Ilemela TARURA
Nae meneja wa TARURA wilaya ya Ilemela Mhandisi Sobe Makonyo ameongeza kuwa mpango wa Serikali ni kuijenga barabara hiyo Kwa kiwango Cha Lami Kwa urefu wa mita 500 kwa kuanzia katika bajeti ya mwaka wa fedha ujao kati ya jumla ya kilomita 1.2 za urefu wote wa barabara hiyo huku ikiwekewa lengo la kuikamilisha yote kwa mwaka wa fedha utakaofuata
Leah Mecksela ni balozi wa CCM wa eneo hilo ambapo amemshukuru na kumpongeza Mbunge Dkt Angeline Mabula kwa kufika katika eneo lake na kuonyesha mfano wa vitendo juu ya utatuzi wa kero ya muda mrefu inayowakabili huku akiomba kupewa kipaumbele kwa wanawake wajasiriamali pindi zoezi la utoaji wa mikopo ya halmashauri litakapoanza