Picha Dereba boda boda na mteja wake wakipita kwa shida katika moja ya barabara zilizoharibiwa na maji ya mvua katika kata ya Msamala Manispaa ya Songea.
Na Mwandishi wetu,
Songea
BAADHI ya wananchi kata ya Msamala Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma,wameiomba serikali kupitia wakala wa barabara za mijini na vijijini(Tarura)wilayani Songea, kufanya matengenezo ya haraka ya miundombinu ya barabara zilizoharibiwa na maji ya mvua ili waweze kuondokana na kero wanazopata ikiwemo kusafirisha wagonjwa.
Walisema,kwa sasa barabara nyingi za mitaa kwenye maeneo hayo ni mbovu hali inayosababisha baadhi ya watu wanalazimika kulipia gharama ya kupaki magari yao kwenye vituo vya mafuta kwa kuwa wanashindwa kufika kwenye makazi yao.
Menald Mwaniti mkazi wa mtaa wa Kiswele alisema,katika kipindi hiki ambacho mvua bado zinaendelea kunyesha kwa wingi, hali inakuwa mbaya zaidi hasa maji yanayotoka barabara kuu ya Songea-Makambako iliyoko chini ya wakala wa barabara Tanzania(TANROADS).
Alisema,katika barabara hiyo kuanzia makutano ya barabara ya Songea Bypass hadi eneo la Mburushi ambalo maji yanapita juu ya barabara badala ya kupita kwenye mifereji na kuelekea upande wa pili kwenye makazi ya watu baada ya mifereji iliyopo kuziba kutokana na kujaa mchanga na takataka
Aidha Mwaniti alisema,barabara za mitaa zilizo chini ya Tarura zimeharibika na hazipitiki kwani hazijafanyiwa ukarabati wowote tangu zilipotengenezwa hivyo kuwa na mashimo makubwa yanayojaa maji na kuhatarisha usalama hasa kwa watoto wadogo.
Mkazi wa mtaa wa Osterbay Hamidu Ramadhan alisema,changamoto kubwa katika mtaa huo ni ubovu wa barabara ambazo zimeharibika kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha kwa wingi katika Mkoa wa Ruvuma.
Hamidu ambaye ni dereva bodaboda alisema,wanakutana na wakati mgumu pale wanapowabeba wateja wao hasa mama wajawazito kuwapeleka kituo cha afya Msamala kwa ajili ya kupata matibabu.
Alisema,wanalazimika kuwashushia njiani badala ya kuwafikisha moja kwa moja kwenye kituo cha kutolea huduma za matibabu kwa sababu ya ubovu wa barabara.
Mkazi wa Msamala Leonald Kapinga alisema,kukosekana kwa mifereji ya kupitisha maji ya mvua katika barabara kuu ya Songea-Makambako ina sababisha mchanga unaosombwa na maji kujaa kwenye makazi yao na hivyo kuingia gharama kubwa ya kuondoa mchanga huo.
Aidha alisema,katika mitaa hiyo kuna wafanyabiashara waliochukua mikopo kutoka kwenye taasisi za fedha na wanatakiwa kufanya marejesho kila wiki, lakini wanashindwa kurejesha kwa wakati kwa kukosa wateja wanaokwenda kununua bidhaa wanazouza kutokana na ubovu wa barabara.
Ameiomba Tarura na Tanroads mkoani Ruvuma,kufanya matengenezo ya barabara zao ili kuwaondolea adha inayowakabili kwani kuna hatari ya kufunga biashara zao kwa kukosa wateja.
Kaimu meneja wa Tarura wilaya ya Songea Godfey Mngale alisema,kabla ya kilio cha wananchi wa Msamala,tayari serikali kupitia Tarura ilishaanza kuchukua hatua kwa kufanya matengenezo ya barabara katika mitaa hiyo.
Mngale alisema,tatizo lililojitokeza kwa sasa ni Mkandarasi amelazimika kusimamisha kazi kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha,lakini mara mvua zitakapokatika kazi ya matengenezo ya barabara katika maeneo hayo zitaendelea kama kawaida.
Amewatoa hofu wananchi wa Msamala kuhusu ubovu wa barabara na kusisitiza kuwa,serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imejipanga kwa kuhakikisha inaboresha miundombinu ya barabara zote ili kurahisisha usafiri na usafirishaji.