Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas kushoto,akikabidhi kombe la Bonanza la Eid el Fitri kwa Nahonda wa Timu ya Kazaroho James James(Akamiko) baada ya timu hiyo kuifunga Timu ya Songea Pamoja goli 1-0 mchezo uliochezwa katika uwanja wa Majimaji mjini Songea.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas,akisalimiana na wachezaji wa Timu ya Songea Pamoja kabla ya kuanza kwa mchezo wa fainali kati ya timu hiyo na Kazaroho uliochezwa katika uwanja wa Majimaji mjini Songea.
Nohadha wa Timu ya Kazaroho James James(Akamiko)akimtambulisha Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas wachezaji wa Timu hiyo kabla ya kuchezwa kwa mchezo wa fainali ya Bonanza la Eid el fitri katika uwanja wa michezo wa Majimaji mjini Songea ambapo Timu hiyo ilifanikiwa kuwafunga wapinzani wake wakubwa timu ya Songea Pamoja kwa goli 1-0.
Na Mwandishi wetu,
Songea
MKUU wa mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas,amefunga Bonanza Eid lililofanyika katika uwanja wa michezo wa Majimaji mjini Songea ambalo wanamichezo wa mkoa huo walitumia bonanza hilo kumkaribisha rasmi mkoani Ruvuma.
Bonanza hilo lilishirikisha timu tano za mpira wa miguu,Timu ya Kazaroho Veterani iliibuka mabingwa baada ya kuwafunga wapinzani wao wakubwa Timu ya Songea Pamoja Goli 1-0 kwenye mchezo wa fainali na kujinyakulia kombe na fedha taslimu Sh.laki tano huku Timu ya Songea Pamoja iliyoshika nafasi ya pili ikipata zawadi ya jezi.
Timu za mpira wa miguu zilizoshiriki bonanza hilo ni Kazaroho,Songea Pamoja,Peramiho Veterani, Songea Veterani na Uvccm Ruvuma,ambapo wana muziki wa kizazi kipya na wasanii wa ngoma za asili wa mkoa wa Ruvuma walitoa burudani kwa wananchi waliofika katika uwanja wa Majimaji.
Kwa upande wa Netiball, timu ya Uvccm wilaya ya Songea iliibuka mshindi wa jumla baada ya kuzifunga timu nyingine nne zilizoshiriki kwenye Bonanza hilo ikiwemo KazaRoho Queen na kupata Sh.laki moja na timu washiriki wa bonanza hilo zilipata jezi seti moja kila moja.
Akizungumza na wananchi na wana michezo walioshiriki katika Bonanza hilo Mkuu wa mkoa,amewapongeza wana michezo walioshiriki na wadau waliowezesha kufanyika kwa bonanza hilo ikiwa ni sehemu ya kusherehekea kumalizika kwa mfungo wa Ramadhani na kusherehekea Sikukuu ya Eid.
Mkuu wa mkoa,amempongeza Mkuu wa mkoa kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya kuwekeza katika sekta ya michezo ambapo uwekezaji huo umesaidia timu za Tanzania kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali.
Mratibu wa Bonanza hilo God Mvulla alisema, huo ni mwanzo tu kwani wadau wa michezo wa mkoa wa Ruvuma wamedhamiria kurudisha heshima ya mkoa wa huo kupitia sekta ya michezo.
Mvulla,ameiomba serikali kupitia wizara ya michezo sanaa na utamaduni kuendelea kuwekeza katika sekta ya michezo ambayo ina mchango mkubwa katika suala la ajira kwa vijana na kuchangia uchumi wa nchi yetu.
Amewataka vijana wa mkoa wa Ruvuma,kushiriki michezo kwani kuna faida nyingi ikiwemo kupata ajira na pia michezo ni afya.