Mkurugenzi wa Huduma za Ushauri na kujenga uwezo kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) Mhandisi Amini Mcharo,akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 9,2024 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa za mafanikio ya miaka mitatu ya Rais Samia na Mageuzi Makubwa katika ununuzi wa Umma nchini.
Na.Alex Sonna-DODOMA
KATIKA kipindi cha Miaka mitatu ya Rais Samia ,Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imefanikiwa kuokoa shilingi Bilioni 16.27 baada ya kufanya uchunguzi kwenye zabuni zilizotekelezwa katika mwaka wa fedha 2021/22 na 2022/23.
Hayo yamesemwa leo Aprili 9,2024 jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Huduma za Ushauri na kujenga uwezo kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) Mhandisi Amini Mcharo wakati akitoa taarifa za mafanikio ya miaka mitatu ya Rais Samia na Mageuzi Makubwa katika ununuzi wa Umma nchini.
Mhandisi Mcharo amesema kuwa Kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni 13.83 ilitokana na kuingilia kati kwa Mamlaka kwenye mikataba ambayo ilitolewa kwa wazabuni wenye bei ya juu wakati wenye bei ya chini wakitolewa kwenye mchakato.
“Kiasi cha shilingi Bilioni 2.44 ni kiasi kilichorudishwa na wasambazaji wa bidhaa na wakandarasi kwa malipo ya ziada yaliyofanywa na Taasisi Nunuzi”amesema Mhandisi Mcharo
Amesema kuwa PPRA imekuwa ikifanya Kaguzi na uchunguzi mbalimbali na mapambano dhidi ya rushwa kwenye taasisi nunuzi.
“Lengo ni kubaini kuwepo kwa ubadhirifu wa fedha za umma, matumizi mabaya ya madaraka na viashiria vya rushwa.Mara baada ya uchunguzi kukamilika, Mamlaka hutoa taarifa zake kwa taasisi nunuzi na kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukuliwa.”amesema
Aidha amesema Mamlaka imewezeshwa kutekeleza vipaumbele mbalimbali katika kusimamia ununuzi wa umma nchini, ambapo imejikita katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya ujenzi wa mfumo wa kielektroniki wa ununuzi wa umma na kuimarisha ufuatiliaji na udhibiti wa ununuzi wa umma.
“Imejikita katika kuwajengea uwezo wadau wa ununuzi wa umma, kutungwa upya kwa Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 10 ya Mwaka 2023, kujenga jengo la ofisi ya makao makuu mkoani Dodoma na kuanzishwa kwa ofisi tano za kanda.”Mhandisi Mcharo
Amesema kuwa Serikali kupitia PPRA, ilianzisha mfumo wa NeST ili kuwezesha michakato yote ya ununuzi wa umma kufanyika kwa njia ya kielektroniki kwa lengo la kuongeza tija, ufanisi, uwajibikaji na uwazi kwenye utekelezaji wa michakato hiyo.
Hata hivyo amesema kuwa “Mfumo wa NeST umeunganishwa na mifumo 17 ya serikali kwa lengo la kuongeza ufanisi, kupunguza muda na gharama za michakato ya ununuzi, kudhibiti vitendo vya udanganyifu, rushwa na kuzuia ukosefu wa maadili.”amesema Mhandisi Mcharo
Amesema kuwa Zaidi ya shilingi trilioni 29 zimewekwa kwenye mfumo wa NeST kwa ajili ya kufanya ununuzi wa bidhaa, huduma na kazi za ujenzi. Hadi kufikia Aprili 09, 2024, mikataba ya zaidi ya shilingi trilioni 5.14 imetolewa kwa wazabuni kupitia mfumo wa NeST, ambapo wazabuni 18,101 wamejisajili kwenye mfumo huo.
Mhandisi Mcharo amesema PPRA imewajengea uwezo makundi maalum na imekamilisha tafsiri ya miongozo miwili inayotumika katika ununuzi wa umma, ambayo ni mwongozo wa ushiriki wa makundi maalum katika ununuzi wa umma na mwongozo wa ushirikishwaji wa jamii katika ununuzi wa umma.
Pia, imetafsiri nyaraka sanifu tatu za zabuni za ushiriki wa makundi maalum katika ununuzi wa umma, nyaraka sanifu ni moja ya zabuni za ushiriki wa jamii katika ununuzi wa umma.
“Hadi kufikia Februari 2024, jumla ya tuzo za mikataba zenye thamani ya shilingi bilioni 1.95 zimetolewa kwa makundi maalum kupitia zabuni za umma zilizotangazwa na taasisi nunuzi kupitia mfumo wa NeST ambapo kundi la vijana wamepata tuzo za mikataba zenye thamani ya shilingi milioni 709, wanawake shilingi bilioni 1.2 na wazee shilingi milioni 78.3.”
Aidha Mamlaka imeandaa sera ya tafiti na agenda iliyoainisha maeneo muhimu ya kufanya utafiti katika ununuzi wa umma. Tafiti zilizokamilika ni kuhusu changamoto na fursa katika ununuzi wa umma na ushiriki wa kampuni za biashara zinazoongozwa na wanawake katika zabuni za umma.
“Mamlaka imekamilisha tafiti ndogondogo katika matumizi ya taratibu ya ununuzi kwa njia ya Force Account ambapo ilibainika kuwa kuna matumizi ya njia hii yasiyoendana na sheria na kanuni inavyoelekeza. Sheria mpya ya ununuzi ya mwaka 2023 imeboresha matumizi ya utaratibu huu.”amesema
Pia ameeleza kuwa Mamlaka ilifanikiwa kusaini hati ya makubaliano na NEEC kwa lengo la kutoa kipaumbele kwa makundi maalumu katika kushiriki fursa zinazotokana na ununuzi wa umma.
Aidha, mamlaka na PCCB zilisaini hati ya makubaliano kwa lengo la kuongeza ushirikiano katika kupambana na rushwa kwenye ununuzi wa umma.
Amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeiwezesha Mamlaka kujenga jengo la ofisi za Makao Makuu jijini Dodoma pamoja na uanzishwaji wa ofisi mpya za kanda tano na hivyo kufanya mamlaka kuwa na ofisi sita za kanda.