Afisa Elimu taaluma Manispaa ya Bukoba Bi. Upendo Nanyaro, akimkabidhi Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mgeza Mseto Bi. Augustina Daniel vitabu vyenye ujumbe muhimu wa lishe kwa watu wasioona vilivyoandaliwa kwa Maandindishi ya nukta nundu (braille) na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania kwa ajili ya kutumiwa na wanafunzi wa wasioona shuleni hapo ili kujifunza masuala mbalimbali yanayohusiana na chakula na lishe
Afisa Mawasiliano Mtafiti wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania, Hamza Mwangomale, akionyesha namna ya kutumia Redio zilizoingizwa ujumbe muhimu wa lishe kwa sauti, kwa ajili ya kusikiliza na watu wasioona, kwa Afisa Elimu Mkoa wa Kagera Bwa. Michael Ligola, mara baada ya kumtembelea ofisini kwake wakati wa zoezi la kugawa na kusambaza vitabu na radio zenye ujumbe muhimu wa lishe kwa watu wasioona vilivyoandaliwa kwa maandishi ya nukta nundu (Braille) Mkoani humo.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watu Wasioona Tanzania Bwa. Omary Itambu, akimkabidhi vitabu vyenye maandishi ya nukta nundu vyenye ujumbe muhimu wa lishe Afisa Elimu Taaluma Manispaa ya Bukoba Bi. Upendo Nanyaro kwa ajili ya kutumiwa na wanafunzi wasioona wa Shule ya Msingi Mgeza Mseto, ili kuweza kujifunza na kupata elimu ya masuala muhimu yanayohusiana na Chakula na Lishe.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watu Wasiiona Tanzania Bwa. Omary Itambu, akimkabidhi Redio zilizoingizwa ujumbe muhimu wa lishe, Afisa Elimu Taaluma Manispaa ya Bukoba Bi Upendo Nanyaro kwa ajili ya kusikiliza na kutumiwa na wanafunzi wasiiona wa Shule ya Msingi Mgeza Mseto, ili kuweza kujifunza na kupata elimu ya masuala muhimu yanayohusiana na Chakula na Lishe.
……………
Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) imekabidhi vitabu 30 na radio 50 zenye ujumbe muhimu wa lishe kwa watu wasioona vilivyoandaliwa kwa maandishi ya nukta nundu (Braille) kwa uongozi wa Shule ya Msingi Mgeza Mseto iliyopo Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera kwa ajili ya kutumiwa na wanafunzi wasioona shuleni hapo.
Nyenzo hizo muhimu kwa watu wasioona zimekabidhiwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watu Wasioona Tanzania (TAB) Bwa. Omary Itambu kwa uongozi wa Shule ya Msingi Mseto na vitatumiwa na wanafunzi wasiona kujifunza na kupata elimu sahihi ya masuala mbalimbali ya lishe kwa kusoma kupitia maandishi ya nukta nundu na kusikiliza kupitia ujumbe wa sauti uliorekodiwa katika redio.
Bwa. Itambu amesema awali walikuwa wanakabiliwa na changamoto ya kupata taarifa na elimu sahihi ya masuala ya afya na lishe kutokana na aina ya ulemavu walionao hivyo kujiona kama kundi ambalo limetengwa katika kupata taarifa hizo muhimu.
“hizi ni nyezo muhimu ambazo tunazikabidhi shuleni kwa ajili ya vijana wetu wasioona kupata elimu ya lishe, ambayo awali walikuwa wanaikosa. Kujifunza kwao kwa sasa kutasaidia kuwafanya kuwa na elimu pana kuhusu masuala ya Chakula na Lishe.” Alisema Itambu
Akipokea vitabu hivyo vyenye maandishi ya nukta nundu na radio zenye ujumbe muhimu wa lishe, kwa niaba ya Afisa Elimu Maalumu Manispaa ya Bukoba, Afisa elimu Taaluma wa Manispaa hiyo Bi Upendo Nanyaro amesema nyezo hizo ni muhimu sana kwa wanafunzi wasioona kwani ndiyo mwanzo wa kuweza kuwasaidia kujua na kutambua masuala muhimu yanayohusiana na Chakula na Lishe.
Kwa Upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mgeza Mseto Bi. Augustina Daniel ameishukuru Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kwa kuwasaidia nyezo hizo muhimu, hivyo kuanzia sasa wanafunzi wake wataweza kupata elimu sahihi ya masuala ya afya na lishe kama ilivyo kwa makundi mengine.
“Wanafunzi wetu hususani hawa wenye mahitaji maalumu wamekuwa wakisahaulika kwenye masuala mbalimbali na hili linatokana na aina ya ulemavu walionao hata hivyo kukumbukwa huku kutasaidia kuona hawajatengwa, na jamii iko pamoja nao katika kuhakikisha inawasimamia katika kutimiza ndoto zao, alisema Bi. Daniel
Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), walifanikiwa kutengeneza na Kuandaa vitabu 500 vyenye maandishi ya nukta nundu na Radio 500 zenye ujumbe muhimu wa lishe kwa Watu wasioona, ili kuweza kufikiwa na elimu ya masuala ya chakula na lishe ambapo mpaka sasa tayari Mikoa ya Singida, Dodoma, Tabora, Njombe, Mwanza na Shinyanga wamekabidhiwa nyezo hizo.