Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akifafanua kuhusu utaratibu wa kurejesha fedha kwa wamiliki wa maduka ya kubadilisha fedha waliobatilishiwa leseni zao baada ya wenye maduka hayo kukidhi vigezo vya kisheria, bungeni jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), alipokuwa akijibu swali bungeni jijini Dodoma la Mbunge wa Chumbuni, Mhe. Ussi Salum Pondeza, aliyetaka kufahamu sababu za maduka ya kubadilisha Fedha kuondolewa katika biashara na wananchi wengi kupoteza ajira zao.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini – Wizara ya Fedha)
Peter Haule na Josephine Majura, WF, Dodoma
Serikali imesema kuwa ilibatilisha leseni za maduka ya kubadilisha fedha za kigeni yaliyokutwa na makosa mbalimbali yakiwemo ya kujihusisha na uhamishaji wa fedha nje ya nchi bila kuwa na leseni wala kibali cha Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Hayo yameelezwa bungeni, jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Chumbuni, Mhe. Ussi Salum Pondeza, aliyetaka kufahamu sababu za maduka ya kubadilisha Fedha kuondolewa katika biashara na Wananchi wengi kupoteza ajira zao.
Mhe. Chande alisema kuwa mwaka 2016, Benki Kuu ya Tanzania ilifanya ukaguzi wa maduka ya kubadilisha fedha za kigeni na kugundua miamala mbalimbali kwa baadhi ya maduka inafanyika kinyume na matakwa ya sheria na kanuni za usimamizi wa maduka ya fedha za kigeni na udhibiti wa utakasishaji wa fedha haramu.
“Mwaka 2018 na 2019, Benki Kuu kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za Serikali ilifanya operesheni ya ukaguzi maalum kwenye maduka yote ya kubadilisha fedha za kigeni nchini na kubaini makosa mbalimbali yaliyosababisha Serikali kusitisha leseni kwa waliokiuka Sheria kwa mujibu wa Kanuni ya 36 (1)(b) na 2 (d) ya Kanuni za Biashara ya Kubadilisha Fedha za Kigeni ya mwaka 2015 iliyorejewa mwaka 2019 ”, alisema Mhe. Chande.
Mhe. Chande alisema kuwa makosa mengine yaliyobainika ni pamoja na kutofanya utambuzi wa wateja kabla ya kutoa huduma kinyume na kifungu cha 15(1) cha Sheria ya Udhibiti wa Utakasishaji Fedha Haramu, Sura 423 na kanuni ya 17 ya Kanuni za Udhibiti wa Utakasishaji Fedha Haramu.
Aidha alisema kuwa kosa lingine lilikuwa kugawa miamala ya wateja kwa lengo la kukwepa kutunza kumbukumbu muhimu zinazoonyesha uhalali wa miamala kinyume na Kanuni ya 23 ya Kanuni za Biashara ya kubadilisha Fedha za Kigeni ya mwaka 2015 na kutokutoa stakabadhi za miamala kinyume na Kanuni ya 23(1) ya Kanuni za Biashara ya Kubadilisha Fedha za Kigeni ya mwaka 2015
Mhe. Chande alibainisha makosa mengine kuwa ni pamoja na kutokuwasilisha taarifa sahihi za miamala Benki Kuu na hivyo kuathiri upatikanaji wa takwimu muhimu kwa ajili ya sughuli za kiuchumi na baadhi ya maduka yalikuwa yanajihusisha na uhamishaji wa fedha nje ya nchi bila kuwa na leseni wala kibali cha Benki Kuu.